Iran yaanza kutekeleza Hatua ya Nne ya kupunguza uwajibikaji wake katika JCPOA
Utekelezaji wa hatua ya nne iliyochukuliwa na Iran ya kupunguza uwajibikaji wake katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA umeanza rasmi leo katika kituo cha nyuklia cha Fordow.
Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (IAEO) limetoa taarifa maalumu likitangaza kuwa: Katika kutekeleza amri ya Rais na Baraza Kuu la Usalama wa Taifa; na kwa usimamizi wa wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), mtungi wa kilo 2,800 uliojazwa ndani yake karibu kilo elfu mbili za gesi ya urani ya heksafloraidi (Gaseous Uranium Hexafluoride, UF6) uliohamishwa kutoka kwenye kinu cha urutubishaji urani cha Natanz umewekwa rasmi kwenye kituo cha nyuklia cha Fordow.
Jana Jumanne, Rais Hassan Rouhani alitangaza utekelezwaji wa hatua ya nne ya kupunguza uwajibikaji wa Iran katika makubaliano ya JCPOA na kusisitiza kuwa: Pande zote katika JCPOA inapasa zitambue kuwa Iran haiwezi kutekeleza peke yake JCPOA.
Dakta Rouhani alisisitiza kwamba: Hatua ya nne ya Iran, kama ilivyo kwa hatua tatu zilizotangulia, nayo pia inaweza kusitishwa na kurejea katika hali ya kabla yake; na endapo pande zote katika JCPOA zitarejea kwenye utekelezaji wa majukumu yao, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nayo pia itatekeleza majukumu yake.
Tarehe 8 Mei 2018 Marekani ilichukua hatua ya upande mmoja ya kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yaliyosainiwa mwaka 2015 kati ya Iran na nchi zilizounda kundi la 5+1.
Baada ya mwaka mmoja tangu ilipojitoa Marekani katika JCPOA na kushindwa nchi za Ulaya kutekeleza ahadi zilizotoa za kufidia athari za vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, Jamhuri ya Kiislamu ilianza kutekeleza hatua kwa hatua upunguzaji wa uwajibikaji wake katika makubaliano hayo.
Kabla ya hatua ya nne iliyochukuliwa jana, upunguzaji wa uwajibikaji katika JCPOA uliochukuliwa na Iran hapo kabla ulikuwa ni pamoja na kuongeza asilimia ya urani iliyorutubishwa hadi 3.67, kuongeza kiwango cha akiba ya urani iliyorutubishwa na kusitisha utekelezaji wa ahadi zote ilizokuwa imetoa katika JCPOA katika uga wa utafiti wa shughuli za nyuklia.../