Nov 14, 2019 11:19 UTC
  • Ayatullah Muhsin Araki
    Ayatullah Muhsin Araki

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu amesema kuwa, kupanuka zaidi ujumbe wa umoja na mshikamano katika Ulimwengu wa Kiislamu na kutengwa mrengo wa mawahabi na matakfiri ni miongoni mwa athari nzuri za ushindi wa kambi ya muqawama na mapambano dhidi ya ubeberu.

Ayatullah Muhsin Araki ameyasema hayo leo katika hutuba yake kwenye Mkutano wa 33 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu. Amesema fikra ya umoja na mshikamano wa Kiislamu imeshinda na kusambaratisha fikra za kitakfiri na mifarakano na kuongeza kuwa: Hii leo suala la kulinda Msikiti wa al Aqsa na Palestina linapaswa kupewa mazingatio makubwa na Waislamu wote kuliko jambo lolote jingine.

Ayatullah Araki amesema kuwa, wadhifa wa Waislamu wa kutetea Palestina umekuwa mzito zaidi katika kipindi cha sasa kwa kutilia maanani njama zinazofanywa na ubeberu na Wazayuni.

Baadhi ya washiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu ametilia mkazo udharura wa kulinda kambi ya mapambano huko Palestina na katika nchi nyingine na kusema: Ushindi mtawalia wa kambi ya mapambano umezidisha uimara wa kambi hiyo.  

Mkutano wa 33 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu mjini Tehran unahudhuriwa na wasomi, wanasiasa, wahadhiri wa vyuo vikuu na wanafikra 400 kutoka nchi 90 duniani.   

Tags