Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu umeanza Tehran kwa kuhudhuriwa na Rais wa Iran
(last modified 2024-09-19T06:48:24+00:00 )
Sep 19, 2024 06:48 UTC
  • Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu umeanza Tehran kwa kuhudhuriwa na Rais wa Iran

Mkutano wa 38 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu umeanza leo hapa mjini Tehran kwa kuhudhuriwa na Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, Mkutano wa 38 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu unaofanyika chini ya kaulimbiu  "Ushirikiano wa Kiislamu ili Kufikia Thamani za Pamoja kwa Kutilia Mkazo Suala la Palestina" umeanza hapa Tehran kwa kuhudhuriwa na wageni 2,500 mbalimbali wakiwemo shakhsia wa kijeshi na pia wasomi na wanafikra wa nchi za Kiislamu. 

Vikao kwa njia ya mtandao vya mkutano huo wa Kiiislamu pia vilianza tangu Jumamosi Septemba 14 na vitaendelea hadi Jumapili Septemba 22.  

Zaidi ya wasomi 230 wa dini na shakhsia wa kitamaduni watatoa hotuba katika kalibu ya mitandao 16 itakayohudhuriwa na watu 15 ambao wameshindwa kushiriki katika Mkutano wa 38 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu hapa Tehran kwa sababu mbalimbali. 

Tarehe 12 Rabiul Awwal mwaka 1446 Hijria ambayo ni sawa na Septemba 16 mwaka 2024 Miladia kwa mujibu wa hadithi, ni siku aliyozaliwa Mtume Muhammad al Mustafa (saw). Waislamu wa Kisuni wanaamini kuwa tarehe 12 Rabiul al-Awwal ni siku aliyozaliwa Mtume Muhammad (s.a.w) huku Waislamu wa Kishia wakiadhimisha  tarehe 17 Rabiul Awwal kuwa  siku ya kuzaliwa Mtume huyo wa rehma.  

Miladun Nabii Mubarak 

Imam Khomeini (M.A) Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye alikuwa mmoja wa shakhsia waliohimiza na kutoa kipaumbele kwa suala la umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu ambapo alitumia suala hili ili kuyaleta pamoja makundi ya Kiislamu na akakitaja kipindi cha baina ya tarehe mbili hizi yaani tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal kuwa wiki ya umoja kati ya Waislamu duniani. 

Wiki hii ni fursa nzuri ya kuchunguza kwa umakini mkubwa haja ya kuwepo umoja na mshikamano katika Ulimwengu wa Kiislamu, hasa katika wakati huu uliojaa fitna na hali ya mchafukoge.

Tags