Rais wa Iran ahitimisha safari yake ya siku tatu ya mazungumzo ya kidiplomasia mjini New York, UN
(last modified 2024-09-26T07:21:38+00:00 )
Sep 26, 2024 07:21 UTC
  • Rais wa Iran ahitimisha safari yake ya siku tatu ya mazungumzo ya kidiplomasia mjini New York, UN

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambaye alisafiri kwenda mjini New York kushiriki katika kikao cha 79 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA), ameondoka mjini humo usiku wa kuamkia leo kurejea Tehran baada ya siku tatu za mikutano na mashauriano ya kina ya kidiplomasia aliyofanya huko.

Jumapili wiki hii, tarehe 22 Septemba, 2024, Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, aliwasili mjini New York akiongoza ujumbe wa ngazi ya juu wa kisiasa kwa lengo la kushiriki katika Mkutano Mkuu wa 79 wa Umoja wa Mataifa na kubainisha misimamo na sera za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa.

Katika asubuhi ya siku ya kwanza ya safari yake mnamo Septemba 23, Rais Pezeshkian alikutana na wakurugenzi na wanahabari waandamizi wa Marekani na wa kimataifa ambapo alikosoa vikali  na kwa uwazi kabisa mashambulizi na jinai za kinyama za utawala ghasibu wa Israel huko Ukanda wa Gaza na kushadidi kwa mashambulizi ya utawala huo katika eneo.

Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran 

Katika siku hiyohiyo ya kwanza ya safari yake mjini New York, Rais wa Iran alikutana na kufanya mazungumzo pia na marais wa Uswisi, Finland, Uturuki na Tajikistan, Mfalme wa Jordan, Rais wa Baraza la Ulaya na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Rais Pezeshkian alikutana pia na wajumbe wa kundi la Wazee au kundi lenye ushawishi, ambalo ni shirika lisilo la kiserikali la viongozi wastaafu wanaofanya kazi kama wanaharakati wa amani na watetezi wa haki za binadamu, wanaojieleza kama viongozi huru wa kimataifa wanaopigania amani na haki za binadamu.

Rais wa Iran alishiriki na kuhutubia pia katika Mkutano wa Kilele wa Mustakabali wa Umoja wa Mataifa, uliofanyika kando ya mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la umoja huo, ambapo alipendekeza Katibu Mkuu wa UN aandae ripoti kamili na jumuishi kuhusu hali ya nchi ambazo ni wahanga wa vikwazo vya kidhalimu na akasema, Iran inataka yafanyike marekebisho ya haraka katika muundo wa uendeshaji wa taasisi za fedha za kimataifa.

Katika siku ya pili ya safari yake mjini  New York, Dakta Pezeshkian alikutana na kuzungumza na kundi la viongozi na wawakilishi wa dini za tauhidi na wanazuoni wa madhehebu ya Shia wanaoishi nchini Marekani, Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Rais wa Serbia na Rais wa Ufaransa.

Ratiba muhimu zaidi ya rais wa Iran katika siku ya pili ya safari yake mjini New York ilikuwa ni kuhutubia kikao cha 79 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA.

Katika siku ya tatu ya safari yake hiyo, Rais Pezeshkian alikutana na wanafikra wakuu wa Marekani, Mwanamfalme wa Kuwait, Waziri Mkuu wa Pakistan, Waziri Mkuu wa Lebanon, Waziri Mkuu wa Norway, Rais wa Bulgaria na Rais wa Baraza la Utawala la Sudan.

Tags