Tuhuma na misimamo ya kurudiwarudiwa ya Marekani kwa ulimi wa Joe Biden katika Umoja wa Mataifa
(last modified 2024-09-26T03:58:08+00:00 )
Sep 26, 2024 03:58 UTC
  • Tuhuma na misimamo ya kurudiwarudiwa ya Marekani kwa ulimi wa Joe Biden katika Umoja wa Mataifa

Jumanne ya wiki hii, rais wa Marekani, Joe Biden, alitoa hotuba yake ya mwisho katika kikao cha 79 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York na kukariri madai ya uongo ya siku zote dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na dhidi ya kambi ya Muqawama. Rais wa Marekani alidai kuwa eti serikali yake inapigania kuleta amani na utulivu katika ukanda wa Asia Magharibi.

Katika hotuba yake hiyo rais huyo kizee wa Marekani amepuuza kabisa jinai za utawala wa Kizayuni za kuwaua shahidi na kidhulma zaidi ya Wapalestina 41,000 katika Ukanda wa Ghaza na badala yake ametoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya HAMAS akidai kuwa harakati hiyo ya Kiislamu imeua na kuteka nyara mamia ya walowezi wa Kizayuni. Amma kuhusu makubaliano ya kusimamisha vita Ghaza, Biden amedai kuwa, hivi sasa makubaliano yanayokubaliwa pia na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa inabidi yatiwe saini, mateka waachiliwe huru ili waweze kurejea majumbani kwao, Ghaza itoke mikononi mwa HAMAS na vita vimalizike.

Biden ametoa tuhuma zisizo na msingi pia kwa Hizbullah ya Lebanon akidai kuwa imerusha makombora na kupiga maeneo ya utawala wa Kizayuni bila ya sababu yoyote akidai kuwa, baada ya kupita karibu mwaka mmoja, watu wengi wa takriban thuluthi mbili za mpakani baina  ya Lebanon na Israel wamekuwa wakimbizi na kwamba vita vya pande zote si kwa manufaa ya yeyote. Amedai kuwa, kutokana na kushadidi mivutano, njia pekee ya kuweza kurejesha usalama wa kudumu na kupelekea kurejea watu majumbani kwao ni njia ya kidiplomasia. Rais huyo wa Marekani  ameashiria pia kupamba moto machafuko dhidi ya Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kudai kwamba, Wapalestina inabidi watatue mgogoro uliopo kwa njia ya kuundwa nchi mbili ili katika nchi yao waweze kuishi kwa usalama na amani.

Jinai za Wazayuni mjini Beirut Lebanon

 

Kimsingi ni kwamba rais huyo wa Marekani hakuwa na jipya katika hotuba yake hiyo aliyoitoa kwenye kikao cha kila mwaka cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Alichofanya ni kurudiarudia misimamo ile ile ya Washington kuhusu matukio ya eneo hili vikiwemo vita vya Ghaza na mashambulizi ya Israel huko Lebanon. Ikiwa ni kuendeleza msimamo ule ule wa Marekani wa kuunga mkono kibubusa na kikamilifu jinai za utawala wa Kizayuni, Biden amedai kuwa makundi ya Muqawama ya Palestina hasa HAMAS na vilevile Hizbullah ya Lebanon eti ndio wasababishaji wa hali iliyopo hivi sasa. Tab'an lengo ni lile lile la kujaribu kuisafisha Israel na jinai zisizo na idadi inazowafanyia Wapalestina hasa mauaji ya kizazi huko Ghaza na hivi sasa mauaji ya wananchi wasio na hatia wa Lebanon kupitia mashammbulizi makubwa na kikatili yanyofanywa na Israel dhidi ya nyumba na makazi ya raia.

Katika hotuba yake hiyo, Biden amedharau kwa makusudi mashambulizi makubwa ya anga ya utawala wa Kizayuni huko Lebanon ambayo yameshaua shahidi zaidi ya watu 600 wasio na hatia na kujeruhi wengine zaidi ya 2500. Ni wazi kwamba kwa mtazamo wa Biden, roho na maisha ya Wazayuni tu ndicho kitu muhimu lakini roho na maisha ya wananchi wa Palestina na Lebanon hayana umuhimu wowote kwake.

Tab'an msimamo huo wa Biden si kitu cha kushangaza sana. Marekani inauunga mkono kikamilifu na kwa pande zote utawala wa Kizayuni; kisiasa, kijeshi, kisilaha n.k, na mshirika wa moja kwa moja na kamili katika kuendelea vita vya Ghaza na mashambulizi makubwa ya utawala wa Kizayuni huko Lebanon pamoja na mauaji ya raia wasio na hatia. Mara chungu nzima serikali ya Biden imekuwa ikitangaza wazi kwamba eti Israel ina haki ya kujilinda na inatumia kisingizio hicho kuusheheneza utawala wa Kizayuni silaha za kisasa kabisa zinazotengenezwa na Marekani zikiwemo ndege za kivita za kizazi cha tano cha F-35. Tab'an siasa hiyo si ya Biden pekee bali naibu wake pia yaani Kamala Harris ambaye ndiye aliyeteuliwa na chama cha Democratia kugombea urais utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu wa 2024 naye pia ni muendelezaji wa siasa hizo. Katika kampeni zake za uchaguzi, Harris amesema bila ya kisisi kwamba siasa za Biden kuhusu kuisheheneza silaha Israel, hazitobadilika iwapo atashinda katika uchaguzi ujao wa rais wa Marekani. 

Mradi wa nyukia wa Iran ni wa amani kikamilifu

 

Suala jingine muhimu katika hotuba ya Biden kwenye Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni tuhuma zake dhidi ya Iran kuhusu mradi wa nyuklia wa Tehran wa matumizi ya amani. Biden amerudia tuhuma zilezile zisizo na msingi na chapwa kwa kudai kuwa eti kuna wajibu wa kukabiliana na vikosi vinavyopigana kwa niaba ya Iran na eti kuizuia Tehran kumiliki silaha za nyuklia.

Tuhuma za Biden kwamba Iran ina nia ya kumiliki silaha za nyuklia zimetolewa katika hali ambayo uhakika kwamba Jamhuri ya Kiislamu haina mpango wowote wa kutumia nishati ya nyuklia kwa malengo ya kijeshi limethibitisha na taasisi kubwa zaidi ya kimataifa ya nyuklia yaani IAEA. Tena wakala huo umethibitisha mara chungu nzima kwamba mradi wa nyuklia wa Iran ni wa amani na ni wa kiraia kikamilifu. Hata mwaka 2022, Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA alikiri hadharani kwa kusema kuwa: "Hatuna ushahidi wowote unaoonesha kuwa hivi sasa Iran ina mpango wa kijeshi wa nyuklia."

Alaakullihaal, tuhuma za madola ya Magharibi kwamba Iran ina mpango wa kumiliki silaha za atomiki hazina msingi wowote. Iran imepiga hatua kubwa katika matumizi salama na sahihi ya nishati ya nyuklia kama kuzalisha umeme, masuala ya matibabu, kilimo na katika nyuga nyinginezo. Mafanikio hayo yanawahamakisha maadui yakiwemo madola ya Magharibi hasa kwa vile lengo kuu hivi sasa la Iran kutumia vizuri zaidi nishati ya atomiki katika kuzalisha umeme.

Tags