Jumatatu, 7 Oktoba, 2024
Leo ni Jumatatu tarehe 3 Mfunguo Siba Rabiul-Thani 1446 Hijria mwafaka na tarehe 7 Oktoba 2024.
Miaka 96 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 16 Mehr mwaka 1307 Hijiria Shamsia kufuatia upinzani wa Sayyid Hassan Mudarres dhidi ya udikteta wa Reza Khan Pahlawi, mtawala huyo aliwaamuru askari wake wavamie nyumba ya Ayatullah Muddares, kumpiga na kumjeruhi na kisha akahamishiwa nje ya mji wa Tehran.
Askari hao pia waliwatia nguvuni watu wa familia ya mwanazuoni huyo. Mwishowe Ayatullah Mudarres alibaidishwa katika mji wa Kashmar kaskazini mashariki mwa Iran na kuuawa shahidi na askari wa Reza Khan mwaka 1316 Hijiria Shamsia.

Katika siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, Ujerumani ya Mashariki iliasisiwa na kuwa na mfumo wa Jamhuri ya Kidemokrasia.
Katika miezi ya mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia, Shirikisho la Umoja wa Sovieti lilivamia na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Ujerumani ya Mashariki, na madola ya Magharibi yakadhibiti sehemu ya magharibi mwa nchi hiyo.
Hata hivyo baadaye Umoja wa Sovieti ulijitoa katika Baraza la Makamanda Waitifaki baada ya kutofautiana na madola ya Magharibi juu ya namna ya kuiendesha nchi hiyo.

Katika siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, utawala wa Baath wa Iraq uliushambulia kwa mabomu ya kemikali mji wa Sumar wa Iran.
Raia wengi waliuawa shahidi katika shambulio hilo. Katika kkipindi cha miaka 8 ya vita vya kichokozi ilivyoansisha dhidi ya Iran, utawala wa Saddam ulitumia mara kkadhhaa silaha za kemikali. Takribani raia laki moja waliuawa shahidi au kujeruhiwa katika tukio hilo la kinyama.

Miaka 23 liyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 7 Oktoba 2001, Marekani iliivamia Afghanistan.
Uvamizi huo ulifanyika kwa kisingizio cha kuliangamiza kundi la wanamgambo wa Al-Qaida ambao kwa mujibu wa Washington walihusika na tukio la Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani.
Katika kipindi cha wiki kadhaa, ndege za kivita za Marekani, zilifanya mashambulizi dhidi ya ngome za kundi la Taliban ambalo katika kipindi hicho lilikuwa likidhibiti eneo kubwa la ardhi ya Afghanistan sambamba na kuliunga mkono kundi la Al-Qaida lililokuwa likiongozwa na Osama bin Laden.
Mashambulizi hayo mazito ya Marekani yaliua na kujeruhi maelfu ya raia wasio na hatia wa Afghanistan huku wengine wakilazimika kuwa wakimbizi.
