Iran yazifungulia mashtaka kanali za Uingereza kwa kuchochea ghasia nchini
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupitia ubalozi wake mjini London, Uingereza imewasilisha mashtaka kwa Idara ya Mawasiliano ya Uingereza OFCOM dhidi ya kanali za upinzani zinazotangaza kwa lugha ya Kifarsi za nchi hiyo, kutokana na kupotosha kwa makusudi matukio ya hivi karibuni nchini hapa.
Hamid Baeidinejad, balozi wa Iran mjini London ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, Tehran imezishitaki kanali hizo za upinzani na ambazo zinatangaza kwa lugha ya Kifarsi kama vile BBC ya Kifarsi, kanali ya Iran International na kanali ya Manoto, kutokana na kupotosha kwa makusudi matukio ya hivi karibuni nchini hapa. Kadhalika amesema kuwa mbali na upotoshaji huo, kanali hizo zimehusika kwa kiasi kikubwa kuchochea ghasia dhidi ya asasi za kiraia nchini Iran na kuitaka Idara ya Mawasiliano ya Uingereza OFCOM kuzichukulia hatua kanali hizo mara moja. Inafaa kuashiria kuwa baada ya kufanyika marekebisho kuhusu bei ya mafuta nchini Iran siku ya Ijumaa wiki iliyopita, wanainchi wa Iran walifanya maandamano ya amani mjini Tehran na baadhi ya miji mingine ya nchi hii. Hata hivyo kundi fulani la wahuni na majangili ambalo lilipata mafunzo kutoka nchi za maadui wa Iran lilijipenyeza kwenye maandamano hayo na kuanza kuharibu mali za umma na za watu binafsi, kushambulia maafisa usalama na polisi na hivyo wakawa wamepotosha na kuteka nyara matakwa halali ya wananchi.
Makundi yanayopinga mfumo wa Kiislamu nchini Iran pamoja na kanali za kigeni zilitumia fursa hiyo na kupitia njama maalumu zikaweza kuchochea ghasia, kueneza propaganda chafu dhidi ya Iran na kuunga mkono wafanya vurugu nchini hapa. Katika uwanja huo kanali ya satalaiti ya Iran International yenye makao yake mjini London, Uingereza ilikuwa na nafasi muhimu katika kurusha moja kwa moja vikao vya makundi ya kigaidi ya Munafiqin (MKO) chini ya uungaji mkono wa kifedha wa Saudi Arabia katika kuchochea ghasia hizo. Aidha kanali ya Manoto ambayo inaendeshwa kupitia fedha zilizoporwa na ukoo wa Mfalme Shah wa Iran kutoka Iran, nayo ilichochea pakubwa ghasia hizo za hivi karibuni nchini hapa.