Mashtaka ya Tehran dhidi ya kanali za Uingereza zinazochochea fujo nchini Iran
Hamid Baeidinejad, Balozi wa Iran mjini London ameandika katika mtandao wa Twitter kwamba, Tehran imezishitaki kanali za maadui wa taifa la Iran za Uingereza ambazo zinatangaza kwa lugha ya Kifarsi kama vile BBC ya Kifarsi, kanali ya Iran International inayofadhiliwa na Saudi Arabia na ile ya Manoto, kutokana na kupotosha kwa makusudi matukio ya hivi karibuni humu nchini.
Wiki iliyopita, baadhi ya miji ya Iran ilikumbwa na fujo za wahuni na maadui wa taifa la Iran baada ya kupandishwa bei ya mafuta humu nchini. Wananchi wa Iran walitumia haki yao ya kidemokrasia ya kuandamana kwa amani kutaka ufafanuzi kuhusu hatua hiyo ya serikali ya kupandisha bei ya mafuta. Hata hivyo maandamano hayo ya amani yalitekwa na wahuni waliochochewa na kanali za satalaiti za mabeberu wa Magharibi hasa Marekani na Uingereza waliofanya fujo na kuharibu mali nyingi za umma na binafsi pamoja na kuwashambulia kwa silaha moto na baridi, raia wa kawaida.
Uchochezi wa vyombo hivyo vya habari ulikwenda sambamba na uadui wa wakuu wa madola ya Magharibi hasa viongozi wa Marekani wa kuunga mkono machafuko na fujo hizo. Kwa kweli, viongozi wa Marekani hawana haya wala junaa kiasi ya kufikia kuchuna nyuso zao na kujifanya eti wanalipenda taifa la Iran na wanaliunga mkono. Baada ya Ikulu ya Marekani, White House pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo kuunga mkono machafuko ya hivi karibuni nchini Iran, hivi sasa mpira amepasiwa Mike Pense, Makamu wa Rais wa Marekani ambaye siku ya Alkhamisi ya tarehe 21 Novemba 2019 alituma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kudai kuwa msimamo wa Marekani uko wazi kwamba wananchi wa nchi hiyo wako pamoja na wananchi wa Iran. Makamu huyo wa rais wa Marekani ametoa madai hayo katika hali ambayo, mara kwa mara, Donald Trump mwenyewe aliwaita wananchi wa Iran kuwa eti ni magaidi. Matamshi hayo ya Mike Pence yametolewa katika hali ambayo vikwazo vya kidhalimu na vya kila upande vya Marekani dhidi ya wananchi wa Iran vimelenga moja kwa moja mahitaji muhimu na ya kimsingi ya wananchi hao hata madawa ya kutibu wagonjwa. Wachambuzi wengi wa mambo wanasema kuwa, viongozi wa Marekani ni waongo na makidhabu kuhusiana na wananchi wa Iran na ndio wahusika wakuu wa moja kwa moja wa matatizo ya hivi sasa ya kiuchumi ya Iran. Si hayo tu, lakini pia siku chache zilizopita, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo, bila soni wala janaa, alitangaza wazi kuwaunga mkono wahuni wanaofanya fujo na kuchoma mali za umma na za watu binafsi nchini Iran huku vyombo vyao vya habari navyo vikiwa mstari wa mbele kuchochea machafuko hayo.
Katika mashtaka yake hayo, Balozi wa Iran mjini London Uingereza amesema, mbali na upotoshaji huo, kanali hizo za utangazaji zimehusika kwa kiasi kikubwa kuchochea ghasia dhidi ya asasi za kiraia nchini Iran na kuitaka Idara ya Mawasiliano ya Uingereza OFCOM kuzichukulia hatua za kinidhamu.
Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nao wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kwamba maadui wa taifa la Iran wamehusika moja kwa moja kwenye fujo na machafuko hayo. Siku ya Jumanne ya tarehe 19 Novemba 2019 wakati akihutubia watu wa sekta ya uchumi humu nchini, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema kwamba, matukio hayo ya hivi karibuni yamefanywa na adui na kamwe hayakufanywa na wananchi. Aidha alisema kuwa vyombo vya habari na taasisi za kipropaganda za mabeberu ni silaha kubwa zinazotumiwa na adui wa uhuru wa mataifa ya dunia, na kwamba kazi yake kubwa ni kuchochea machafuko katika mataifa ya dunia.
Kusema kweli hii si mara ya kwanza kwa vyombo vya habari vya mabeberu kuchochea machafuko nchini Iran na haitarajiwi kuwa mara yao ya mwisho. Katika machafuko ya mwaka 2009 pia vyombo vya habari vya mabeberu vilichochea mno fujo nchini Iran. Wakati huo Msemaji wa Wizara ya Hazina ya Marekani, alitangaza wazi uungaji mkono wa machafuko ya nchini Iran na alisema: Kama yalivyoonesha matukio ya Iran, mawasiliano binafsi ya Intaneti kama vile Email, Chat na mitandao ya kijamii, ni silaha zenye nguvu sana.
Siku zote ndoto ya Marekani ni kuona kunatokea machafuko nchini Iran ili itoe pigo kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, lakini ndoto zake hizo kamwe hazitoaguliwa kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.