Waziri wa TEHAMA Iran: Vikwazo vya Marekani haviwezi kuzuia maendeleo Iran
Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano nchini Iran mapema Jumamosi ametoa kauli baada ya jina lake kuwekwa katika orodha ya vikwazo vya Marekani na kusisitiza kuwa, Washington haiwezi kuzuia maendeleo na ustawi nchini Iran.
Mohammad Javad Azari Jahromi, katika ujumbe aliotuma kwa njia ya Twitter amesema si yeye peke yake aliyewekewa vikwazo bali mashirika kadhaa ya kiteknolojia ya startups, watengenezaji programu za kompyuta, wagonjwa wa saratani na watoto wanaougua ugonjwa wa ngozi wa EB ni kati ya waliowekewa vikwazo na Marekani.
Azari Jahromi amebaini kuwa ataendelea kuunga mkono upatikanaji huru wa intaneti.
Wagonjwa wa ngozi wa Epidermolysis Bullosa kwa kifupi EB ni ugonjwa nadra wa kurithi ambao huathiri ngozi na wanaougua ugonjwa huo hukabiliwa na hatari kubwa ya kupata saratani.
Hadi hivi sasa watoto 15 Wairani ambao wanaougua ugonjwa huo wamepoteza maisha kutokana na vikwazo vya dawa ambavyo Marekani imeiwekea Iran.
Siku ya Ijumaa Wizara ya Fedha ya Marekani, ikiwa ni katika muendelezo wa uraibu wa vikwazo wa nchi hiyo, ilitangaza kumuweka Waziri wa Iran wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika orodha yake ya vikwazo.

Wizara ya Fedha ya Marekani imemuwekea vikwazo Waziri Azari Jahromi kwa kisingizio kuwa amebana na kufunga intaneti nchini Iran.
Katika siku za hivi karibuni, wakuu wa Marekani wamekuwa wakidai kuwa Iran imekata intaneti ili kuzuia kile wanachodai ni kufika sauti ya 'waandamanaji' nje ya nchi. Hii ni katika hali ambayo Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran limeamua kukata intaneti kutokana na uzoefu wa huko nyuma wa uchochezi wa mashirika ya kijasusi ya ajinabi hasa mashirika ya kijasusi ya Marekani na utawala wa Kizayuni katika ghasia hasa katika fitina za mwaka 2009 na ghasia za mwaka 2017.
Itakumbukwa kuwa, Ijumaa iliyopita, serikali ya Iran iliamua kukata ruzuku ya mafuta iliyokuwa ikiitoa. Pamoja na kuondolewa ruzuku hiyo, bado Iran ni miongoni mwa nchi ambazo bei ya mafuta ya petrol ni ya chini zaidi duniani ambapo kwa sasa lita moja ya petroli kwa watumizi wa kawaida ni takribani senti 14 za Kimarekani. Maandamano ya kualalmikia hatua hiyo yalitumiwa vibaya na wahuni kuibua ghasia na machafuko nchini. Katika siku za hivi karibuni wananchi wa Iran wameandamna kulaani ghasia hizo.