Kamanda Mkuu wa IRGC: Iran inazidi kung'ara duniani
-
Meja Jenerali Hossein Salami
Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amehutubia kongamano la kikosi cha kujitolewa hapa nchini (Basiji) cha watu elfu 10 mkoani Hamedan, magharibi mwa nchi na kubainisha kwamba, hii leo Iran ni kitivo cha matukio ya kisiasa na kwamba inadhibiti masual yote ya kioperesheni na kung'ara duniani.
Sambamba na kubainisha kwamba taifa la Iran lina uelewa na halikubali ila kujitawala amesema kuwa, katika uwanja wa vita vya kiuchumi adui anaelekea kushindwa katika ndoto zake za kuuangusha uchumi wa nchi hii na kuifanya Tehran isalimu amri mbele yake. Kwa mujibu wa Meja Jenerali Hossein Salami, adui alifikiria kwamba angeipigisha magoti nchi hii lakini kile kinachoshuhudiwa ni kwamba adui huyo ameshindwa na raia wa Iran. Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ameongeza kwamba Iran ina utaalamu wa kuwashinda maadui na kwamba maadui hao watafeli katika kila uga.
Amesisitiza kwamba hii leo Marekani ni mfumo uliopooza na wenye maradhi ya kupoteza kumbukumbu na kubainisha kuwa, mfumo wa kisiasa wa Marekani unakusudia kuyashusha na kuyarejesha nyuma mataifa mengine ya dunia na kwamba kushirikiana na serikali khabithi ya Washington hakuwezi kuifanya nchi mshirika kufikia malengo na fakhari yake. Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) sambamba na kubainisha kwamba kikosi cha kujitolea cha wananchi (Basij) ni ngao ya taifa hili amesema kuwa, kikosi hicho ni muujiza wa Mwenyezi Mungu, zao la fikra za Ki-Mungu kwenye moyo wa Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini (MA) na mti bora ambao chini ya Kiongozi Muadhamu umezidi kuenea ndani ya moyo na roho ya taifa la Iran.