Rais Rouhani awatumia viongozi wenzake duniani salamu za mwaka mpya 2020 Miladia
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewatumia ujumbe wa pongezi marais na viongozi na mataifa ya Wakristo kwa mnasaba wa kuanza mwaka mpya wa Miladia wa 2020.
Katika ujumbe wake wa mwaka mpya, Dakta Rouhani amesema, "Natumai kwamba, katika mwaka huu unaoanza, viongozi wa dunia wataimarisha ushirikiano wao na kusimama dhidi ya ubeberu, sanjari na kuchukua maamuzi ya kauli na vitendo kwa misingi ya sheria na uhuru, pamoja na kuufanya mpya huu uwe wa amani kwa wanadamu wote."
Rais Rouhani mbali na kuwatakia Wakristo duniani mwaka mpya wenye baraka, utulivu na amani amebainisha matumaini yake kuwa, viongozi wa dunia wataweza kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazoyakabili mataifa yao.
Kadhalika Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran, Eshaq Jahangiri pia ametuma ujumbe wa kheri na fanaka kwa mnasaba wa kuanza mwaka huu mpya wa 2020 Miladia. Amewatakia watu wote duniani hususan wafuasi ya dini ya Kikristo kutoka kila rangi, dini na kaumu mwaka mpya uliojaa afya, amani na utulivu.
Leo tarehe Mosi Januari inayosadifiana na kuanza mwaka mpya wa 2020 Miladia, ni siku kuadhimisha mwaka mpya katika jamii za Wakristo na nchi nyingi za Afrika, America, Ulaya, Australia na hata Asia.
Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, IRIB, linawatakia Wakristo wote duniani, hasa Wakristo wa hapa nchini Iran, mwaka uliojaa baraka, utulivu na amani.