Iran yaitaka Marekani iachane na sera zake haribifu katika eneo
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameionya Marekani juu ya matokeo mabaya ya hatua zake haribifu na zisizo na mantiki katika eneo la Asia Magharibi.
Abbas Mousavi amesema madai ya watawala wa Washington kuwa kuna mkono wa Iran katika maandamano na ghasia zinazoshuhudiwa nchini Iraq hivi sasa hayana msingi na ni tusi kwa taifa la Iraq.
Huku akiitaka kukomesha siasa zake haribifu katika eneo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameihutubu Marekani kwa kuihoji, "Imetumia mantiki gani kudhani kuwa Wairaqi wangenyamazia kimya jinai zao na kukanyaga uhuru wa kujitawala nchi hiyo?"
Amewakumbusha Wamarekani kuwa, hawapaswi kusahau kuwa Wairaqi wanawatazama kama wavamizi ndani ya nchi hiyo huku akionya kuwa, chokochoko zozote watakazochukua zitakabiliwa na jibu kali na wananchi wa Iraq.
Wakati huohuo, Majid Takht-Ravanchi, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema, madai hewa ya Marekani dhidi ya Iran yanalenga kuisahaulisisha dunia kuhusu uvamizi wao dhidi ya Iraq kwa kipindi cha miaka 17, uliosababisha mauaji ya Wairaqi 300,000 wasio na hatia.
Hapo jana, Rais Donald Trump aliendeleza bwabwaja zake kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwa kuandika: "Iran imeua mwanakandarasi Mmarekani na kujeruhi wengine kadhaa. Tumetoa jibu kali, na daima tutaendelea kutoa (majibu). Iran itabeba dhima kwa njama zake za kushambuliwa ubalozi wa Marekani mjini Baghdad."
Hii ni katika hali ambayo, wananchi wa Iraq jana Jumanne walifanya maandamano katika ubalozi huo wa Marekani mjini Baghdad, ambapo mbali na kuteketeza moto lango la kuingia kwenye ubalozi huo na bendera za Marekani, walisikika wakipiga nara za kutaka kuondoka nchini humo askari vamizi wa Kimarekani.