Ukraine: Hitilafu za ufundi ndizo zilizoangusha ndege yetu karibu na Tehran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i58387-ukraine_hitilafu_za_ufundi_ndizo_zilizoangusha_ndege_yetu_karibu_na_tehran
Ubalozi wa Ukraine mjini Tehran umesema kuwa, hitilafu za kiufundi ndizo zilizopelekea kuanguka ndege ya nchi hiyo karibu na mkoa wa Tehran, hapa nchini Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 08, 2020 07:41 UTC
  • Ukraine: Hitilafu za ufundi ndizo zilizoangusha ndege yetu karibu na Tehran

Ubalozi wa Ukraine mjini Tehran umesema kuwa, hitilafu za kiufundi ndizo zilizopelekea kuanguka ndege ya nchi hiyo karibu na mkoa wa Tehran, hapa nchini Iran.

Ndege moja ya abiria ya Shirika la Ndege la Ukraine leo asubuhi imeanguka karibu na Uwanja wa Ndege wa Imam Khomeini MA hapa Tehran.

Shirika la habari la IRNA limeunukuu ubalozi huo wa Ukraine ukikanusha madai kwamba ndege hiyo imeangushwa katika shambulio la kigaidi la kombora na kusisitiza kuwa, kuharibika injini ya ndege hiyo ndiko kulikoifanya ianguke.

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine naye amezitahadharisha pande zinazoeneza habari za uongo kuhusu ajali hiyo na kuzitaka ziache mara moja kufanya hivyo.

Mabaki ya ndege ya abiria ya Shirika la Ndege la Ukraine iliyoanguka leo Jumatano, Januri 8, 2020 karibu na mkoa wa Tehran

 

Wakati huo huo Bw. Qassem Biniyaz, mkuu wa Kituo cha Mawasiliano na Upashaji Habari cha Wizara ya Barabara na Ujenzi wa Miji ya Iran amesema kuwa, sababu iliyopelekea ndege hiyo kuanguka ni moto uliotokea kwenye injini yake.

Naye pia amekanusha vikali madai kwamba ndege hiyo aina ya Boing 737 ya Shirika la Ndege la Ukraine, imetunguliwa kwa kombora na kusisitiza kuwa, kama ndege hiyo ingelitunguliwa kwa kombora basi ingeliripuka huko huko angani, lakini moto uliotokea kwenye injini yake na kushindwa rubani kuidhibiti ndege hiyo ndiko kulikoifanya ianguke na kupelekea kufariki dunia watu waliokuwemo.

Ndege hiyo ilikuwa na abiria 167 na wahudumu 9. Wengi wa abiria hao walikuwa ni raia wa Iran.