Raisi: Marekani ikituvamia tutavitimua vikosi vyake Ghuba ya Uajemi
Mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Iran ameonya dhidi ya tishio lolote la adui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kubainisha kuwa, iwapo Washington itathubutu kuchukua hatua yoyote iliyo dhidi ya Iran basi taifa hili litawatimua hadi chini ya Ghuba ya Uajemi wanajeshi wa Marekani.
Sayyid Ebrahim Raisi alisema hayo jana katika hotuba yake mbele ya vikosi vya jeshi la Iran katika mji bandari wa Bushehr, kusini mwa nchi na kueleza bayana kuwa, "Wamarekani wakichukua hatua yoyote yenye ishara za tishio, shambulio au uvurugaji wa uthabiti dhidi ya Iran, vikosi shupavu vya Iran likiwemo Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na vikosi vya kujitolea wananchi vya Basiji vitawasukuma chini ya Ghuba ya Uajemi."
Mkuu wa Idara ya Mahakama nchini Iran ameongeza kuwa, hakuna chembe ya shaka kuwa majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu yatatoa pigo na jibu kali na kuibuka mshindi mkabala wa wavamizi.

Huku akivipongeza vikosi vya Iran kwa kuimarisha usalama katika eneo la Asia Magharibi, Sayyid Ebrahim Raisi amebainisha kuwa, majeshi ya Iran katu hayataruhusu Wamarekani na nchi za Ulaya zitishie usalama wa watu wa eneo hili.
Amesema, "uwepo wa majeshi ya Iran umewakosesha usingizi Wamarekani katika eneo (Asia Magharibi)."
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikionya mara kwa mara dhidi ya hatua yoyote ya adui ya kuivamia kijeshi nchi hii ikisisitiza kuwa, uvamizi wowote utajibiwa kwa nguvu zote na vikosi vya usalama vya taifa hili.