IRGC iko tayari kivita kukabiliana na corona nchini Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i59788-irgc_iko_tayari_kivita_kukabiliana_na_corona_nchini_iran
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amewapongeza madaktari na wafanyakazi wa sekta ya afya nchini Iran kutokana jihadi yao isiyo na kikomo katika kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19 (corona) na kusema: "Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu liko tayari kivita nchini Iran kukabiliana na kirusi cha corona."
(last modified 2026-08-29T06:03:32+00:00 )
Mar 16, 2020 22:11 UTC
  • IRGC iko tayari kivita kukabiliana na corona nchini Iran

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amewapongeza madaktari na wafanyakazi wa sekta ya afya nchini Iran kutokana jihadi yao isiyo na kikomo katika kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19 (corona) na kusema: "Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu liko tayari kivita nchini Iran kukabiliana na kirusi cha corona."

Kamanda Mkuu wa IRGC Brigedia Jenerali Hussein Salami ameyasema hayo Jumatatu alipotembelea Kituo cha Vita vya Kibiolojia katika Kamandi Kuu ya IRGC mjini Tehran ambapo alifanya mazungumzo kwa njia ya video na makamanda wote wa IRGC nchini ambao wamewasilisha ripoti kuhusu hatua walizochukua katika vita dhidi ya corona.

Meja Jenerali Salami ametoa wito kwa wananchi kufuata ushauri wa wizara ya afya ili kuangamiza corona huku akieleza matumaini kuwa hivi karibuni wananchi wa Iran watashuhudia mwisho wa kirusi hicho.

Aidha amesema Majeshi ya Iran yanatekeleza oparesheni ya kuwatafuta na kuwatenga katika karantini walioambukizwa corona kote nchini.

Siku ya Ijumaa Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Iran Meja Jenerali Mohammad Baqeri alisema: " Wananchi wote wa Iran watachunguzwa kupitia intaneti, simu na ikilazimu, kufika sehemu aliko mtu, na wale wote wanaoshukiwa kuwa na ugonjwa huo watatambuliwa."

Magari ya Majeshi ya Iran yakiwa tayari kuelekea katika oparesheni ya kukabiliana na corona

Amesema wanaoshukiwa kuwa na corona watapelekwa katika vituo vya afya na kwamba Majeshi ya Iran yataanzisha vituo zaidi ya 1,000 vya matibabu ya wagonjwa wa corona.

Siku ya Alhamisi Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Alhamisi alitoa amri kwa Meja Jenerali Mohammad Baqeri Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kutaka kamandi hiyo iunde 'Kituo cha Afya na Matibabu' kwa lengo la kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19.