Moscow yakosoa mienendo isiyo ya kibinadamu ya Marekani mkabala wa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i59905-moscow_yakosoa_mienendo_isiyo_ya_kibinadamu_ya_marekani_mkabala_wa_iran
Russia imeitaka Marekani kukomesha mienendo yake isiyo ya kimaadili ya kuiwekea vikwazo Iran hasa kwa kutilia maanani kipindi cha sasa cha maambukizi ya virusi vya corona. Wito huo wa Moscow ni sehemu ya upinzani wa kimataifa dhidi ya vikwazo haramu na vinavyokiuka sheria vya Marekani dhidi ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 22, 2020 20:47 UTC
  • Moscow yakosoa mienendo isiyo ya kibinadamu ya Marekani mkabala wa Iran

Russia imeitaka Marekani kukomesha mienendo yake isiyo ya kimaadili ya kuiwekea vikwazo Iran hasa kwa kutilia maanani kipindi cha sasa cha maambukizi ya virusi vya corona. Wito huo wa Moscow ni sehemu ya upinzani wa kimataifa dhidi ya vikwazo haramu na vinavyokiuka sheria vya Marekani dhidi ya Iran.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Ryabkov amekariri tena upinzani wa serikali ya Moscow kwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran na kusema kuwa: "Russia inaitaka Marekani ikomeshe mienendo yake isiyo ya kibinadamu na vikwazo vya upande mmoja dhidi ya Iran." 

Ryabkov ameashiria hali ya sasa ya maambukizi ya virusi vya corona nchini Iran na kusema: "Tehran inakabiliwa na uhaba wa vifaa kwa ajili ya kutatua matatizo ya kiafya katika kipindi cha sasa cha mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona." 

Wito huo wa Russia wa kuondolewa vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Iran katika kipindi cha sasa cha kasi ya maambukizi ya virusi vya corona katika pembe mbalimbali za dunia unafuatia miito kama hiyo iliyotolewa na viongozi wa nchi mbalimbali zikiwemo Uturuki, Ujerumani, Lebanon, Pakistan na China.

Siku chache zilizopita pia Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Muhammad Javad Zarif alisema: Ugaidi wa kimatibabu na kiuchumi wa Marekani unatatiza mapambano athirifu ya Iran dhidi ya maambukizi ya virusi hivyo vinavyoenea kwa kasi duniani. 

Vilevile Ijumaa iliyopita Rais Hassan Rouhani  wa Iran alisema kuwa: Siasa za uono finyu na za uhasama zitazolenga kudhoofisha mfumo wa utabibu na kuviwekea mpaka vyanzo vya fedha vya kushughulikia hali iliyoko Iran zitakuwa na athari ya moja kwa moja kwa mchakato wa kupambana na janga la dunia nzima la corona katika nchi zingine.

Rais Hassan Rouhani

Rais Rouhani aliongeza kuwa, wakati umefika kwa wananchi wa Marekani kupaza sauti zao kwa kuhoji na kutaka majibu kwa serikali yao na akawaambia: Msikubali nyaraka za historia ya Marekani zizidi kuwa chafu kuliko ilivyo hivi sasa.