Jeshi la Iran lapokea ndege za kivita zisizo na rubani
Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limepokea ndege mpya za kivita zisizo na rubani ambazo zina uwezo wa kutekeleza oparesheni kadhaa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Habari la IRIB, sherehe za kukabidhi ndege hizo za kivita zisizo na rubani au drone zimehudhuriwa na Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Amir Hatami. Katika sherehe hizo, Jeshi la Iran limekabidhiwa aina mbili za drone ambazo ni 'Karrar' na 'Ababil-3' na drone za mwendo kasi zenye injini aina ya 'Jet' zenye uwezo wa kutekeleza majukumu kadhaa.
Akizungumza wakati wa kukabidhi ndge hizo, Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema: "Zana hizi zimeundwa kwa kutegemea uwezo wa ndani ya nchi unojumuisha wataalamu Wairani katika viwanda vya ulinzi, vyuo vikuu na mashirika ambayo msingi wake ni elimu."
Brigedia Jenerali Hatami amesema ndege zisizo na rubani ambazo zimezinduliwa zina sifa za kipekee na zinaweza kufuatilia kwa karibu, ikiwa ni pamoja na kuchukua picha za harakati za maadui katika maeneo yote ya Iran. Hali kadhalika amesema drone hizo zina uwezo wa kusheheni mabomu na makombora na hivyo zinaweza kutumika katika oparesheni za kivita.
Waziri wa Ulinzi wa Iran pia ameashiria uwezo wa drone hizo kuruka katika masafa ya juu sana na kusema: "Drone hizi zinaweza kuruka juu masafa ya mita 40,000 hadi 45,000 sambamba na kutekeleza oparesheni katika eneo la umbali wa kilomita 1500.