Apr 21, 2020 07:59 UTC
  • Zarif: Iran inashirikiana na UN kuhitimisha matatizo ya Wayemen

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema nchi hii inashirikiana na Umoja wa Mataifa katika jitihada za kuhakikisha kuwa matatizo na changamoto zinazowakabili wananchi wa Yemen zinafikia tamati.

Muhammad Javad Zarif amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa mtandano wa kijamii wa Twitter jana usiku na kuongeza kuwa,  Iran haitachoka kuchukua hatua za kuimarisha amani katika eneo hili la Asia Magharibi.

Katika ujumbe huo, Dakta Zarif ameandika: Katika jitihada zetu za kudumisha amani katika eneo na vita dhidi ya ugaidi; Leo nimekutana na Rais Assad na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria kabla ya mkutano wa Astana kwa njia ya video.

Zarif ameashiria kuhusu jitihada za Iran za kurejesha amani na uthabiti nchini Afghanistan na kusema kuwa, mwakilishi maalumu wa Iran alikutana na wawakilishi wa pande zote husika mjini Kabula siku chache zilizopita.

Kuhusu matatizo ya Wayemen, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema mwakilishi maalumu wa Iran anashirikiana na UN na Wayemen kuhakikisha kuwa matatizo yanayowakabili wananchi wa nchi hiyo maskini ya Kiarabu yanapatiwa ufumbuzi.

Waziri Zarif alipokutana na Rais Bashar wa Syria jana

Kwa mujibu wa taasisi ya utafiti ya Marekani ya Armed Conflict Location and Event Data Project (ACLED), vita vya Yemen vimeua watu zaidi ya 100,000 hadi sasa. Saudia kwa kushirikiana na waitifaki wake wanaishambulia na kuizingira Yemen kwa kutumia silaha za Wamagharibi tokea Machi 2015.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ambaye jana alifanya safari ya siku moja nchini Syria alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa nchi hiyo Bashar al-Assad pamoja na Walid al-Muallim Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Syria, ambapo walijadili masuala mbalimbali ya pande mbili, kieneo na kimataifa.

Tags