Apr 24, 2020 02:45 UTC
  • Iran yalaani chokochoko za Marekani Ghuba ya Uajemi, yamuita balozi wa Uswisi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa vikali chokochoko za jeshi la Marekani dhidi ya wanajeshi wa baharini wa Iran katika Ghuba ya Uajemi, sambamba na kukosoa bwabwaja na vitisho vya Rais Donald Trump dhidi ya askari hao wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH).

Katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa Twitter jana Alkhamisi, Mohammad Javad Zarif alisema vikosi vya Marekani vinawachokoza kwa makusudi mabaharia wa Iran katika Ghuba ya Uajemi. 

Akizungumza hivi karibuni na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House, Trump alidai kuwa tayari ameshawaamrisha wanajeshi wa Marekani kushambulia boti za Iran zilizopo katika Ghuba ya Uajemi iwapo watachokozwa.

Dakta Zarif ameshangazwa na kauli hiyo ya Trump na kusema: Jeshi la Marekani halina biashara yoyote umbali wa maili 7,000 toka nyumbani, na kuja kuwachokoza mabaharia wetu katika fukwe za Ghuba yetu ya Uajemi.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amejibu pia ujumbe wa Twitter wa Trump unaosema #Jeshi la Marekani limekumbwa na visa zaidi ya 5,000 vya Covid-19, na kuandika: Donald Trump anapaswa kushughulikia mahitaji yao (wanajeshi wa US), badala ya kutoa vitisho huku akishangiliwa na magaidi wa Saddam.

Boti za Iran zikipita karibu na manowari za Marekani katika Ghuba ya Uajemi

Wakati huo huo, Iran imemuita Balozi wa Uswisi hapa Tehran, Markus Leitner na kumkabidhi malalamiko rasmi ya taifa hili dhidi ya harakati za kichokozi za vikosi vya Marekani katika Ghuba ya Uajemi. 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Abbas Mousavi amesema mwakilishi huyo wa maslahi ya Marekani hapa nchini amekumbushwa juu ya umuhimu wa kuheshimu sheria na kanuni za kimataifa za ubaharia na uhuru wa kutembea boti na meli. Kadhalika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa onyo kali na kusema kuwa itajibu kwa nguvu zote vitisho na chokochoko zozote zilizo kinyume cha sheria katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman. 

Tags