IRGC: Vikwazo vya Marekani havijasimamisha ustawi wa elimu nchini Iran
Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran IRGC amesema kuwa kurushwa satalaiti ya kijeshi ya Iran iliyopewa jina la Nour-1, katika anga za mbali, kumeonyesha kwamba, vikwazo haramu vya Marekani havijazuia maendeleo ya kielimu nchini Iran.
Satalaiti ya Nour-1 ambayo ni satalaiti ya kwanza ya kijeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ilirushwa angani siku ya Jumatano kupitia roketi la Qased na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC kutokea katikati mwa Iran kwenda umbali wa kilometa 425. Kufuatia hatua hiyo Brigedia Jenerali Ramazan Sharif, Msemaji wa IRGC sambamba na kubainisha kwamba satalaiti hiyo ya Nour-1 ni mafanikio ya vijana wa Iran, amesema kwamba, kwa mara ya kwanza maadui wote baada ya hatua hiyo, wamekiri juu ya mafanikio makubwa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika anga za mbali. Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Wamarekani na Ulaya wamekiri kwamba vikwazo havijaweza kutia dosari yoyote katika ustawi wa kielimu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Amebainisha kuwa licha ya vikwazo vikali kabisa, lakini vijana wa Iran na kwa azma na irada wameweza kufikia mafanikio makubwa ya kielimu. Brigedia Jenerali Ramazan Sharif pia ameashiria hatua za Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika kukabiliana na virusi vya Corona na kufafanua kuwa, kwa kuzingatia mapendekezo ya idara ya kitaifa ya kupambana na Corona, tangu siku za mwanzo jeshi la IRGC lilikabidhi hospitali zake kwa Wizara ya Afya ya Iran sambamba na kuanzisha vituo vingi vya matibabu. Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Kiislamu amesema kuwa vikosi vya kujitolea Basij, na Jeshi la IRGC viliingia kazini na kupuliza dawa ya kuua vijidudumaradhi katika vituo vya umma zikiwemo hospitali. Pia amesema vimeanzisha kituo cha Imam Hassan (as) ambapo kufikia sasa vimetoa mamilioni ya vifurushi vya msaada wa chakula kwa zaidi ya familia milioni tatu.