Iran: Marekani haina misingi ya kisheria kujifanya mshiriki wa JCPOA
(last modified Sun, 03 May 2020 08:11:33 GMT )
May 03, 2020 08:11 UTC
  • Iran: Marekani haina misingi ya kisheria kujifanya mshiriki wa JCPOA

Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Taasisi za Kimataifa mjini Vienna amesema jitihada za Marekani za kutaka kuionesha dunia kuwa ingali mshiriki wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA hazina misingi ya kisheria.

Kazem Gharibabadi amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake wa Twitter huku akirejelea kipengee cha 10 cha Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kinachoashiria kuwa iliacha kuwa mshiriki wa JCPOA mnamo Mei 8 mwaka 2018, baada ya rais wa nchi hiyo Donald Trump kujitoa bila ya sababu katika mapatano hayo ya kimataifa.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Iran amenukuu waraka wa Trump wa kuiondoa Marekani kwenye makubaliano hayo ya nyuklia, ambapo sehemu moja ya waraka huo inasema: Marekani imesitisha kivitendo ushiriki wake kwenye JCPOA kuanzia sasa Mei 8 mwaka 2018.

Hivi sasa utawala wa Trump unafanya njama za kuhakikisha kuwa Umoja wa Mataifa hautekelezi kivitendo mapatano hayo na wala azimio la umoja huo lililopasisha kuondolewa Iran vikwazo vya silaha ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu wa 2020.

Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Taasisi za Kimataifa mjini Vienna amesema licha ya Washington kutoshiriki kikao chochote kilichofanyika katika fremu ya JCPOA, lakini imekuwa ikifanya jitihada za makusudi za kuyasambaratisha mapatano hayo na hata kutishia kuziadhibu nchi zinazofanya biashara na Iran.

Trump alipoindoa US kwa kiburi kwenye JCPOA mwaka 2018

Hivi karibuni pia, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa alisema Marekani haina hoja ya kisheria ya kutaka kuwa mshirika wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, na kwamba jitihada za Washington za kutaka kuishinikiza Iran kwa kutumia azimio nambari 2231 zitagonga mwamba.

Kadhalika nchi nyingi duniani zikiwemo za Ulaya pamoja na Russia zimetangaza bayana kupinga kuongezwa muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran. 

Tags