Rouhani: Iran haitakubali ukiukwaji wa azimio 2231
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Tehran katu haitakubali ukiukwaji wowote wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Ameongeza kuwa: "Ni haki isiyopingika ya Iran kuwa, vikwazo vya silaha viondolewe dhidi yake hivi karibuni katika fremu ya azimio hilo."
Akizungumza leo Jumatano katika kikao cha baraza la mawaziri, Rais Rouhani ameashiria jitihada za Marekani za kutaka kurefushwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran na kusisitiza kuwa: "Kuondolewa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran ni kati ya nukta zisizopingika katika JCPOA."
Rais wa Iran ameongeza kuwa: "Iwapo vikwazo vya silaha vitarejeshwa kwa anwani yoyote au kwa mbinu yoyote ile, viongozi wa kundi la 4+1 wanafahamu matokeo mabaya yatakayowakumba."
Hali kadhlika Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema iwapo Iran inanunua au inauza silaha, ni kwa ajili ya kuyahami na kuyalinda mataifa na kwamba Iran haitumii silaha zake kwa ajili ya uchochezi au kuanzisha vita.
Rais Rouhani aidha ameashiria kumbukumbu ya kujiondoka Marekani katika mapatano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) na kusema: "Mnamo Mei 8 mwaka 2018, Rais Donald Trump wa Marekani alichukua hatua ya kijinga na ya upande mmoja ya kujiondoa katika JCPOA." Rais wa Iran amesema Trump aliiondoa nchi yake katika JCPOA kutokana na chuki zake binafsi dhidi ya rais aliyemtangulia Barack Obama, ambaye aliidhinisha mapatano hayo, na pia kutokana na mashinikizo ya wenye misimamo mikali ndani ya Marekani na pia kutokana na mashinikizo ya utawala wa Israel na Saudi Arabia.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameendelea kusema kuwa, baada ya miezi miwili, Wamarekani waliamka kutoka katika mghafala na kugundua kuwa wamefanya kosa kubwa kwa kujiondoa katika JCPOA.
Rais Rouhani amesisitiza kuwa, Wamarekani hawako tena katika mapatano ya JCPOA isipokuwa tu wawasilishe ombi kwa wanachama wa JCPOA na kisha baada ya hapo wafidie makosa yote waliyoyafanya sambamba na kuondoa vikwazo vyote.