UN kuingilia kati hatua ya Marekani kupora dola bilioni za Iran
Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema yuko tayari kuutafutia ufumbuzi mgogoro kati ya Iran na Marekani kuhusu hatua ya Washington kuzuia mali za Tehran katika benki zake.
Akijbu barua ya Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Ban amesema ofisi yake iko tayari kuingilia kati juu ya mzozo huo iwapo pande zote husika zitaonyesha utayarifu wao.
Akithibitisha kupokea barua hiyo, Stephane Dujarric, Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa: "Ofisi ya Katibu Mkuu daima iko wazi na tayari kwa ajili ya kuipatia ufumbuzi mizozo ya aina yoyote."
Jumatano ya Aprili 20, Mahakama Kuu ya Marekani ilipitisha uamuzi kuwa katika kuchunguza madai ya waathirika wa eti makosa ya jinai za ugaidi, mahakama za nchi hiyo zinaweza kutumia mali na fedha za Iran zilizozuiliwa nchini humo ili kuwalipa fidia watu hao.
Katika mahojiano na gazeti la The New Yorker siku ya Jumatatu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliashiria hukumu hiyo na kusema: "Huo ni wizi, ni wizi mkubwa, ni uharamia na hakuna shaka tutachukua tena udhibiti wa fedha hizo."
Mahakama hiyo ilisema dola bilioni mbili za Iran zilizoko katika benki za Marekani zipewe familia za wanajeshi wa Marekani waliouawa mwaka 1983 katika hujuma ya bomu mjini Beirut Lebanon ambapo Iran inatuhumiwa kuhisika nayo.