Iran yaapa kutoa jibu kali kwa chokochoko za kijeshi za Marekani
Iran itatoa jibu kali kwa chokochoko za kijeshi za Marekani baada ya Rais Donald Trump kutumia turufu yake kupinga azimio la Bunge la Kongresi la hatua ya kijeshi isichukuliwe dhidi ya Iran kabla ya idhini ya wabunge.
Hayo yamesemwa na Balozi wa Iran nchini Russia Kazem Jalali katika mahojiano na shirika la habari la Sputnik. Balozi Jalali amesema hatua ya Trump ilikuwa na malengo mawili ya kutaka kujihakikishia ushindi katika uchaguzi ujao wa rais na kuwa huru katika maamuzi ya kuanzisha hujuma ya kijeshi dhidi ya Iran.
Balozi wa Iran nchini Russia ameionya vikali Marekani kuhusu kuanzisha chokochoko yoyote ya kijeshi dhidi ya Iran huku akisisitiza kuwa Washington itakabiliwa na jibu kali.
Siku ya Jumatano Trump alitumia kura yake ya turufu na kukataa kuidhinisha azimio ambalo lilipitishwa na Baraza la Wawakilishi na Baraza la Seneti katika Bunge la Kongresi. Azimio hilo lilikuwa limemuwekea rais huyo wa Marekani vizingiti katika kuanzisha vita dhidi ya Iran.
Azimio hilo liliwasilishwa na chama cha upinzani cha Democrat baada ya Trump kuamuru kuuawa kigaidi Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Luteni Jenerali Qassem Soleimani mnamo Januari 3.
Katika mahojiano hayo, Balozi Jalali amesema Iran imepokea mapendekezo kutoka nchi kadhaa kuhusu ununuzi wa silaha. Amesema Iran inalenga kuchukua hatua kadhaa kuimarisha uwezo wake wa kijeshi baada ya vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa kuondolewa dhidi yake mwezi Oktoba.