Iran yapeleka Denmark mashine za kuzalisha barakoa
Makamu wa Rais wa Iran wa Masuala ya Sayansi na Teknolojia amesema Jamhuri ya Kiislamu imepeleka nchini Denmark mashine za kuzalisha barakoa za kujikinga virusi vya corona.
Sorena Sattari alisema hayo jana Jumatano hapa jijini Tehran na kuongeza kuwa, vifaa vinavyohitajika katika mahospitali kwa ajili ya kukabiliana na corona vinatengezwa na wataalamu na mashirika ya hapa nchini.
Jana pia, Parviz Karami afisa katika Ofisi ya Makamu wa Rais wa Iran wa Masuala ya Sayansi na Teknolojia alisema mbali na kuuza nje ya nchi mashine za kuzalisha barakoa, lakini taifa hili limeziuzia nchi mbalimbali duniani barakoa aina ya N95.
Wiki iliyopita, Kamati ya Kielimu ya Idara ya Kitaifa ya Kupambana na virusi vya Corona nchini Iran ilisema kuwa nchi 40 zimetuma maombi ya kutaka kununua vifaa vya kubaini Corona ambavyo vimetengenezwa na Shirika la Kielimu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Mapema mwezi huu wa Mei, shehena ya kwanza ya vifaa vya kubaini ugonjwa wa Covid-19 vilivyotengenezwa na shirika moja lenye msingi wa elimu nchini Iran inayojumuisha vifaa elfu 40 vya kupimia corona ilipelekwa nchini Ujerumani.
Nchi kadhaa zikiwemo Ujerumani, Uturuki, Poland na mataifa kadhaa ya Amerika Kusini zimeomba kuuziwa vifaa hivyo vya kubaini virusi vya Corona.
Hivi sasa Iran haiagizi nje ya nchi vifaa vya aina yoyote kwa ajili ya kukabiliana na corona; na kwa sasa vifaa vyote vya hospitali, Vyumba vya Wagonjwa Mahututi (ICU) na sehemu nyinginezo vinaundwa na kuzalishwa humu humu nchini na mashirika ya ndani.