Usalama wa Ghuba ya Uajemi kwa mtazamo wa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i61304-usalama_wa_ghuba_ya_uajemi_kwa_mtazamo_wa_iran
Iwapo eneo la Ghuba ya Uajemi litakuwa salama, nchi zote za eneo hilo zitafaidika na usalama huo, kinyume chake, nchi zote za eneo hilo zitakumbwa na ukosefu wa usalama iwapo Ghuba ya Uajemi haitakuwa salama.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 30, 2020 06:58 UTC
  • Usalama wa Ghuba ya Uajemi kwa mtazamo wa Iran

Iwapo eneo la Ghuba ya Uajemi litakuwa salama, nchi zote za eneo hilo zitafaidika na usalama huo, kinyume chake, nchi zote za eneo hilo zitakumbwa na ukosefu wa usalama iwapo Ghuba ya Uajemi haitakuwa salama.

Akitembelea jana Ijumaa awamu ya mwisho ya uundaji na ukamilishaji wa manowari ya Dena na ile ya kutegua mabomu baharini ya Saba huko  Bandar- Abbas kusini mwa Iran, Waziri wa Ulinzi wa Iran Amir Hatami amesisitiza kuwa: "Nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi zina jukumu la kudhamini na kudumisha usalama wa eneo hilo, na hatua ya nchi jirani kuiruhusu Marekani kuingia Ghuba ya Uajemi ni kosa la kistratejia." 

Siasa za Iran kuhusu usalama wa eneo hilo zimejengeka kwa mujibu wa sera ya usalama wa jumuishi na kwa msingi huo Iran inaamini kuwa kuweko hali ya mchafukoge katika eneo la Ghuba ya Uajemi kuna madhara kwa nchi zote za eneo hilo. Usalama wa Ghuba ya Uajemi pia unataliwa na msingi huo. Stratejia ya Iran kwa ajili ya kudumisha amani na utulivui katika eneo la Ghuba ya Uajemi inaweza kuchambuliiwa katika pande mbili.

Upande wa Kwanza unajumuisha stratejia za kiusalama kwa ajili ya kukabiliana na vitisho vya moja kwa moja dhidi ya usalama wa nchi. Katika uwanja huo, sera ya kijeshi ya Iran imebainishwa wazi  kwa misingi wa kujilinda na kukabiliana na vitisho kutokea kwenye mipaka ya Iran. Upande wa pili wa stratejia ya usalama ya Iran unasisitiza suala la kushirikiana nchi za eneo na kanda hii. 

Boti za kushambulia kwa makombora zilizokabidhiwa kwa jeshi la Sepah 
 

Stratejia mbili hizi kwa pamoja ni muhimu kwa ajili ya kuwa na eneo lenye amani na utulivu kwa maslahi ya pamoja ambayo si tu ni dharura kwa usalama katika Ghuba ya Uajemi pekee bali kwa ajili ya ulimwengu mzima. 

Katika kukabiliana na vitisho mbalimbali vikiwemo vita na ugaidi  na pia ukosefu wa usalama baharini, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka kushirikiana na kushirikishwa nchi zote za eneo la Ghuba ya Uajemi katika mipango ya pamoja ya kiusalama; na wakati huo huo inapinga wazi misimamo ya nchi moja ya kutumia mabavu dhidi ya nchi nyingine. 

Vikosi vya jeshi la majini la Iran vinalinda kikamilifu usalama katika Ghuba ya Uajemi na viko tayari kukabiliana na vitisho dhidi ya nchi hii. Aidha vimedhihirisha uwezo wake kwa kuimarisha usalama ndani ya maji ya nchi na nje ya mipaka.  

Meja Jenerali Hossein Salami Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH naye alisisitiza juzi Alhamisi katika sherehe za kukabidhiwa jeshi hilo boti 100 za kushambulia kwa makombora huko Bandar Abbas, kuwa Iran inataka kupanua wigo wa nguvu zake za kiulinzi hadi maeneo ya mbali na kusema kuwa: Kikosi cha Majini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, SEPAH, hivi sasa kina jukumu la kupanua wigo wa nguvu za kiulinzi baharini za kuyaimarisha Mapinduzi ya Kiislamu na Jamhuri ya Kiislamu. 

Meja Jenerali Hossein Salami 

Kuwepo meli za Iran katika njia kuu za uchumi wa dunia huko kaskazini mwa bahari ya Hindi na kutekeleza majukumu yake katika Bahari ya Atlantic kunadhihirisha uwezo waIran katika sekta za baharini. Umuhimu wa uwezo huu wa Iran ni katika kalibu ya sera ya kiulinzi ya Iran kwa ajili ya kuzuia kutokea vita.

Tajiriba ya karibu karne moja inaonyesha kuwa, nchi ajinabi siku zote zimekuwa chanzo cha ukosefu wa amani katika Ghuba ya Uajemi na sababu ya mivutano katika eneo hilo. Si hayo tu bali nchi hizo zimekuwa zikidai kuwa Iran ni tishio kwa usalama na chanzo cha mivutano katika eneo la Ghuba ya Uajemi ili zipate fursa ya kuzifanya tegemezi nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi  katika suala la usalama na hivyo ziuze silaha zao za mabilioni ya dola na kuvilinda vituo vyao vya kijeshi katika eneo hilo.   

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi kuanzisha vita katika kanda hii au nje ya eneo hili lakini itatetea usalama wake kwa nguvu zote iwapo itakabiliwa na vitisho au kuchokozwa.