Wabunge wa Iran walaani 'ugaidi wa kibaguzi' wa polisi ya Marekani
(last modified Wed, 03 Jun 2020 03:55:09 GMT )
Jun 03, 2020 03:55 UTC
  • Wabunge wa Iran walaani 'ugaidi wa kibaguzi' wa polisi ya Marekani

Wabunge 240 wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) wametoa taarifa ya kulaani mwenendo wa polisi ya Marekani wa kutumia ugaidi wa kibaguzi dhidi ya raia wa nchi hiyo.

Wabunge hao wameashiria juu ya kuuawa kinyama na polisi mzungu, Mmarekani mwenye asili ya Afrika na kusema kuwa: Kwa mara nyingine tena, ugaidi wa kibaguzi wa polisi ya Marekani dhidi ya mtu mweusi asiye na ulinzi umefungua pazia na kuweza wazi hulka ya ukatili ya utawala wa Marekani. George Floyd ni mmoja kati mamia ya Wamarekani wenye asili ya Afrika wanaouawa kila mwaka na polisi ya Marekani.

Taarifa hiyo ya Wabunge wa Iran imeeleza kinagaubaga kuwa: Raia weusi nchini Marekani wameshindwa kupumua kwa miongo kadhaa sasa kutokana na ugaidi wa kibaguzi nchini humo, video ya kuuawa kikatili George Floyd si tu imepaza sauti ya kilio cha raia weusi, lakini pia imepaza sauti ya Wamarekani wote wanaonyongeshwa huku wakisema 'hatuwezi kupumua'.

Aidha watunga sheria hao wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran wamesema matukio yanayoshuhudiwa hivi sasa nchini Marekani yamefichua ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu nchini humo, na kwamba hatua ya rais gaidi wa Marekani kutishia kuwaua waandamanaji inaashiria kuwa, watu wa nchi nyinginezo duniani si wahanga pekee wa ugaidi wa kiserikali wa Marekani, lakini pia raia wa Marekani ndio wahanga wa kwanza wa ugaidi huo wa kidola.

Ugaidi wa kiserikali wa US haumsazi yeyote

Maafisa mbalimbali wa ngazi za juu wa Iran wakiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif, Sayyid Ebrahim Raisi, Mkuu wa Chombo cha Mahakama nchini Iran na Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, wametoa taarifa za kulaani ubaguzi wa rangi na ukatili huo wa kutisha wa polisi ya Marekani.