Imam Khomeini na uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu na nchi nyingine
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i61382-imam_khomeini_na_uhusiano_wa_jamhuri_ya_kiislamu_na_nchi_nyingine
Licha ya Imam Khomeini (MA) kusisitiza juu ya mapambano na kusimama imara dhidi ya madola ya kibeberu na kiistikbari, lakini pia alikuwa na msimamo wa wazi kifikra juu ya kuwa na uhusiano mzuri na nchi nyingine za dunia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 03, 2020 02:12 UTC
  • Imam Khomeini na uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu na nchi nyingine

Licha ya Imam Khomeini (MA) kusisitiza juu ya mapambano na kusimama imara dhidi ya madola ya kibeberu na kiistikbari, lakini pia alikuwa na msimamo wa wazi kifikra juu ya kuwa na uhusiano mzuri na nchi nyingine za dunia.

Msimamo wa kwanza na muhimu kuhusu fikra hiyo ya Imam (MA) ni kuwa na uhusiano mzuri na nchi za Kiislamu kwa msingi wa 'Umma mmoja wa Kiislamu' badala ya kuzingatia utaifa katika uhusiano huo. Imam (MA) hakuupa umuhimu mkubwa utaifa na ukabila katika uhusiano wake na mataifa ya Kiislamu bali alizingatia udharura wa kuwa na 'Umma mmoja wa Kiislamu' katika uhusiano huo. Anasema kuhusu suala hilo: 'Uislamu ni taifa moja na nchi za Kiislamu zinakaribiana, kama ilivyo mitaa tofauti ya mji mmoja. Wote (Waislamu) wana jukumu la kushikamana na kuwa chini ya bendera ya Uislamu kwa msingi wa sheria za Kiislamu. Wanawajibika kuwa na msimamo mmoja katika kukabiliana na wale wanaopinga Uislamu.'

Katika uwanja huo, Profesa Ruhullah Ramadhani, mhadhiri wa Kiirani katika vyuo vikuu vya Marekani anasema: Imam Khomeini alikuwa akipinga sana misimmamo mikali ya utaifa wa moja kwa moja kwa sababu ilikuwa ikiudhuru ulimwengu wa Kiislamu na nukta hii inapaswa kuzingatiwa kuwa maslahi na utukufu wa Uislamu ndio unaopasa kuainisha siasa za serikali za Kiislamu na sio maslahi ya kitaifa moja kwa moja.'

Imam Khomeini (MA), Imam wa Umma wa Kiislamu

Msingi mwingine muhimu wa fikra ya Imam Khomeini katika kuwa na uhusiano na nchi nyingine ni kuheshimiana pande mbili. Imam, Mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu alilipa umuhimu mkubwa suala la kuwa na uhusiano bora na mataifa ya kigeni katika siasa za nje lakini wakati huo huo akisema kuwa uhusiano huo ulipasa kusimama juu ya msingi wa kuheshimiana pande mbili. Kuhusu hilo alisema: 'Uhusiano wetu na nchi zote za kigeni utasimama juu ya msingi wa heshima ya pande mbili. Kuhusu hili, hatutakubali kudhulumiwa wala sisi kumdhulumu yeyote.'

Ni kwa msingi huo ndipo akapinga vikali sheria ya Capitulation katika zama za utawala wa Shah Pahlavi katika uhusiano wake na Marekani, ambapo hakuna raia yeyote wa Marekani aliyefanya kosa au kuhusika na uhalifu wa aina yoyote nchini hapa aliyapasa kuhukumiwa katika mahakama za Iran, bali alitakiwa kuhukumiwa nchini Marekani tu. Katika kipindi cha Mapinduzi ya Kiislamu pia alisisitiza sana juu ya kuwa macho taifa na kutetea kwa nguvu zake zote mwamko wa Kiislamu.

Msingi mwingine muhimu wa uhusiano wa Imam Khomeini na mataifa ya kigeni ulikuwa udharura wa kufikiwa amani na usalama katika mataifa hayo. Imam alisisitiza sana juu ya kulindwa msingi huo kutokana na mafundisho ya Uislamui na nafasi yake kama mwanazuoni mkubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Alikuwa akisema: 'Taifa na serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaheshimu sheria tukufu za Qur'ani na Uislamu. Kwa mujibu wa mafundisho ya Qur'ani Tukufu, Iran ni ndugu wa imani wa mataifa yote ya Kiislamu na pia wa nchi nyinginezo kwa msingi wa utamaduni na jografia. Inataka kuishi pamoja kwa amani na serikali na mataifa yote. Itaichukulia kuwa ndugu, nchi yoyote ambayo haitavamia nchi nyingine na kuheshimu sheria za Uislamu.'

Mazishi ya kihistoria ya Imam Khomeini (MA)

Msingi mwingine muhimu wa fikra ya Imam Khomeini kuhusu suala la kuwa na uhusiano mzuri na mataifa mengine ni kutoingilia mambo ya ndani ya nchi hizo. Msingi huo ni moja ya misingi muhimu zaidi ya mitazamo ya Imam Khomeini kuhusu siasa za nje. Kwa hakika kwa mtazamo wa Imam Khomeini (MA), imani hupatikana tu pale nchi zinapoamua kutoingilia masuala ya ndani ya upande wa pili. Anasema kuhusu jambo hilo: 'Ninatumai kwamba amani itapatikana ulimwenguni pale nchi zitakapojitawala, kutoingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine, kulinda ardhi za nchi za eneo na kutochokozwa nchi za ulimwengu wa tatu na za Kiislamu na hasa za eneo hilo, kinyume cha sheria.'

Msingi huu muhimu wa fikra ya Imam Khomeini kuhusu siasa za kigeni unavunjilia mbali madai yote yasiyo na msingi yanayotolewa na madola ya kibeberu ya Magharibi na vibaraka wao katika eneo kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaingilia mambo ya ndani ya nchi za eneo na kuchochea ghasia na mivutano katika eneo la Asia Magharibi.