Waliopona COVID-19 nchini Iran wapindukia 125,000
Wizara ya Afya, Matibabu na Mafunzo ya Tiba ya Iran imetangaza kuwa, hadi hivi sasa waathirika 125,206 wa ugonjwa wa COVID-19 au corona humu nchini Iran wamepona na kuruhusiwa kurejea nyumbani kutoka mahospitalini.
Daktari Kianoush Jahanpour, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari ya Wizara ya Afya ya Iran ametangaza hayo leo Jumatano katika kikao cha kila siku na waandishi habari na kuongeza kuwa wagonjwa wapya 3,134 wa COVID-19 wamegundulika Iran katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita.
Daktari Jahanpour ameongeza kuwa kwa ujumla watu walioambukizwa COVID-19 nchini Iran ni 160, 696.
Daktari Jahanpur hali kadhalika ameashiria kufariki dunia wagonjwa 70 wa corona nchini Iran katika kipindi cha masaa 24 hadi kufikia leo mchana na kusema kuwa, hadi sasa watu 8,012 wameshafariki dunia kwa COVID-19 humu nchini.
Aidha amesema kuwa, hadi sasa kumefanyika vipimo karibu milioni moja vya kubaini ugonjwa wa COVID-19 nchini.
Idadi jumla ya walioambukizwa COVID-19 duniani hadi kufikia sasa ni milioni 6,4 na waliopoteza maisha ni karibu 383,000. Marekani inaongoza duniani kwa maambukizi na vifo vya corona ambapo hadi kufikia leo watu 1,881,256 walikuwa wameambukizwa COVID-19 na wengine zaidi ya 108,062 wamepoteza maisha.