Watu zaidi ya 127,000 walioambukizwa COVID-19 nchini Iran wapona
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i61416-watu_zaidi_ya_127_000_walioambukizwa_covid_19_nchini_iran_wapona
Wizara ya Afya ya Iran imetangaza kuwa, hadi hivi sasa waathirika 127,485 wa ugonjwa wa COVID-19 au corona nchini Iran wamepona na kuruhusiwa kurejea nyumbani kutoka mahospitalini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 04, 2020 21:55 UTC
  • Watu zaidi ya 127,000 walioambukizwa COVID-19 nchini Iran wapona

Wizara ya Afya ya Iran imetangaza kuwa, hadi hivi sasa waathirika 127,485 wa ugonjwa wa COVID-19 au corona nchini Iran wamepona na kuruhusiwa kurejea nyumbani kutoka mahospitalini.

Daktari Kianoush Jahanpour, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari ya Wizara ya Afya ya Iran ametangaza hayo jana Alhamisi katika kikao cha kila siku na waandishi habari na kuongeza kuwa wagonjwa wapya 3,574 wa COVID-19 wamegundulika Iran katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita kufikia jana adhuhuri.

Daktari Jahanpour amesema baina kesi mpya za maambukizi zilizoripotiwa, 493 wamelazwa hospitaliani na 3,080 wamepata matibabu bila kulazwa na kwamba kwa ujumla watu walioambukizwa COVID-19 nchini Iran ni 164,270.

Daktari Jahanpour hali kadhalika ameashiria kufariki dunia wagonjwa 59 wa corona nchini Iran katika kipindi cha masaa 24 hadi kufikia jana adhuhuri na kusema kuwa, hadi sasa watu 8,071 wameaga dunia kwa COVID-19 hapa nchini.

Wafanyakazi wa sekta ya afya Iran wakionyesha azma ya kukabiliana na corona

Amesema kuwa, hadi sasa kumefanyika vipimo karibu milioni moja  na 19 elfu vya kubaini ugonjwa wa COVID-19 nchini. 

Idadi jumla ya walioambukizwa COVID-19 duniani hadi kufikia Alhamisi ilikuwa ni takribani milioni 6,6 na waliopoteza maisha ni zaidi ya 388,500. Marekani inaongoza duniani kwa maambukizi na vifo vya corona ambapo hadi kufikia leo watu 1,903,868 walikuwa wameambukizwa COVID-19 na wengine zaidi ya 109,176 wamepoteza maisha.