Russia yalaani vitisho vya Marekani dhidi ya Iran
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema kuwa hatua ya Marekani ya kuzitishia nchi na pande zote zinazosahilisha usafirishaji wa mafuta ya Iran kuelekea Venezuela ni jambo lisilokubalina na linalopaswa kulaaniwa.
Maria Zakharova amesema vitisho vya Marekani vya kuziwekea vikwazo nchi zinazorahisisha usafirishaji wa mafuta ya petroli ya Iran kwenda Venezuela havikubaliki. Zakharova amekemea sera za vikwazo za Marekani na ameongeza kuwa, Moscow inatoa wito wa kukomeshwa hatua zinazokiuka sheria za serikali ya Washington.
Hivi karibuni Wizara ya Fedha ya Marekani ilitangaza kuwa, imeyawekea vikwazo makampuni manne ya meli yaliyohusika kusafirisha mafuta ya Iran kwenda Venezuela na kutishia kuwa, nchi, viongozi wa bandari, wamiliki na manahodha wa meli zitakazosafirisha mafuta ya Iran kwenda Venzuela watawekwa kwenye orodha ya vikwazo ya Marekani.
Katika jitihada za kuisaidia nchi inayozingirwa kiuchumi na Marekani ya Veneuela, hivi karibuni Jamhuri ya Kiislamu ilituma meli kubwa tano zinazobeba nishati na mafuta nchini humo na meli hizo zote zimewasili salama na kutia nanga licha ya vitisho vya serikali ya Washington.
Hatua hiyo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi hiki ambapo nchi zote mbili za Iran na Venezuela zimewekewa vikwazo vya Marekani, imewakasirisha sana viongozi wa serikali ya Washington.