Namaki aipongeza Iran kwa mapambano yake dhidi ya Corona
Waziri wa Afya wa Iran Saeed Namaki ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu kwa jinsi ilivyoshughulikia tatizo la maambukizi ya virusi vya corona hapa nchini akisema taifa hili sasa limekuwa muuzaji nje wa vifaa na zana za tiba baada ya kuwa muagizaji kutoka nje wa vifaa madawa licha ya vikwazo haramu vya Marekani.
Saeed Namaki amesema hayo kupitia njia ya video katika uzinduzi wa kiwanda ya kuzalisha mada zinazotumiwa katika viwanda vya kutengenza madawa ya binadamu katika mkoa wa Markazi. Kiwanda hicho ni cha kwanza cha aina yake eneo la magharibi mwa Asia.
Waziri Namaki amesema Iran imeokoa Yuro milioni 700 katika mwaka uliomalizika wa Kiirani kwa kutumia dawa na bidhaa za kuzalisha madawa zilizozalishwa ndani ya nchi.
Amesema jambo muhimu zaidi ni kwamba, Iran ambayo imeathiriwa na vikwazo vya kidhalimu, imeweza kudhibiti maambukizi ya corona katika kipindi cha siku 60 na kubadilika kuwa muuzaji wa bidhaa na vifaa vya tiba nje ya nchi baada ya kuwa muagiza wa bidhaa hizo.
Iran ni miongoni mwa nchi zilizoathiriwa na virusi vya corona vilivyoanzia katika mji wa Wuhan nchini China Disemba mwaka jana na kuzagaa katika pembe mbalimbali za dunia.
Wakati huo huo Msemaji wa Wizaya ya Afya ya Iran Kianoush Jahanpour amesema kuwa watu 2,364 wameambikizwa virusi vya corona katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita hapa nchini na kwamba 72 miongoni mwao wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo.
Marekani inaongoza duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya wahanga na waarhiriwa na virusi vya corona. Zaidi ya Wamarekani 112,101 wmefariki dunia kutokana na ugonjwa huo.