Udharura wa mabadiliko katika Idara ya Mahakama kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu
Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Jumamosi alizungumza moja kwa moja kwa njia ya video na mkuu na maafisa wa ngazi za juu wa Idara ya Mahakama ya Iran ambapo alimuenzi shahidi madhulumu Ayatullah Baheshti, Shahidi Qodossi, Shahidi Ladjevardi na mashahidi wengine wa Idara ya Mahakama ya Iran.
Akizungumza katika kikao hicho, Ayatullah Khamenei alisema: "Kutayarishwa waraka mpya na ulioimarika wa mabadiliko katika Idara ya Mahakama' kwa kutegemea wasomi, wanazuoni na watu wenye uzoefu katika idara ya mahakama ni hatua yenye thamani kuwa.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu amesema kuleta mabadiliko ni kazi ngumu sana kivitendo na huku akiashiria njama zisizo na kikomo za maadui zenye lengo la 'kuvuruga kila harakati ya mabadilko na mageuzi katika mfumo' kupitia propaganda za vyombo vya habari na kuibua wasi wasi na mtazamo mbaya katika fikra za umma, amesisitiza kuwa: "Njia pekee yenye taathira katika kukabiliana na wanaopinga marekebisho ni kutositisha harakati, kuwa na istiqama, kumtegemea Mwenyezi Mungu na kuendelea kwa ushujaa katika mkondo wa mabadiliko."
Kiongozi Muadhamu katika hotuba yake pia amesisitiza kuhusu jukumu muhimu la Idara ya Mahakama na udharura wa kukabiliana na wafisadi na wale wote wanaojihusisha na ubadhirifu wa mali ya umma na kutumia vibaya madaraka. Hali kadhalika Kiongozi Muadhamu amesisitiza ulazima wa nchi nzima kuchukua tahadhari pande zote ikiwa ni pamoja na kukabiliana na uhasama wa Marekani na Uingereza khabithi na hali kadhalika kukabiliana na hatua za serikali za Ulaya. Kiongozi Muadhamu ameendelea kusema: "Kama tutatekeleza ipasavyo majukumu yetu, basi kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu njama zao zote zitafeli, watashindwa kufikia malengo yao na matokeo ya mashinikizo ambayo wenyewe wanajigamba kuwa ni ya kiwango cha juu kabisa yatakuwa ni kushindwa maadui hao na kuchezea kipigo kutoka kwa taifa la Iran na mwishowe watalazimika kulegeza misimamo yao na kurudi nyuma."
Kupambana na ufisadi na ukosefu wa uadilifu si jambo jipya. Matakwa ya wananchi katika nchi mbali mbali ikiwa ni pamoja na Marekani yanaoonyesha kuwa, kuwepo uadilifu kunahitaji marekebisho katika sheria za kibaguzi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria hotuba ya rais wa Marekani ambaye ameamuru wanaovunja masanamu ambayo ni nembo ya ubaguzi wafungwe miaka 10 jela au kutenganishwa watoto na wazazi wao wahajiri, na kusema huu ni ukiukwaji wa sheria ambao unafichwa na vyombo vya habari vya kipropaganda vya nchi za Magharibi.
Kiongozi Muadhamu katika sehemu nyingine ya hotuba yake amesema kuna sababu nyingi za kuibuka ufisadi na ukosefu wa uadilifu katika jamii na moja ya sababu hizo ni udhaifu wa vyombo vyenye majukumu ya ukaguzi, kutoeleweka sheria na taratibu na mfumo mbovu wa kiidara, ukiritimba na usimamizi mbovu katika sekta ya uchumi. Kiongozi Muadhamu amesema hali kama hii haikubaliki hata kidogo katika mfumo wa mahakama za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hivyo wasimamizi wanatakiwa kuleta mabadiliko yanayoenda sambamba na mahitajio pamoja na ustawi wa Idara ya Mahakama. Amesema mchakato wa uadilifu unapaswa kuanza kwa nguvu na kupewa uzito maradufu katika zama mpya za 'Hatua ya Pili ya Mapinduzi."
Ni kwa msingi huo ndio hotuba ya Kiongozi Muadhamu kuhusu vyombo vya mahakama kufanya kazi bila mapendeleo ina nukta muhimu zitakazosaidia kufikiwa mabadiliko katika Idara ya Mahakama.
Kiongozi Muadhamu pia katika siku zilizopita wakati alipokuwa akitangaza mkakati wa kistratijia wa 'Hatua ya Pili ya Mapinduzi' alisisitiza kuwa: "Uadilifu na kupambana na ufisadi ni nukta mbili za lazima na zinazohitajiana. Ufisadi wa kiuchumi, kimaadili na kisiasia ni dhihirisho la uchafu katika nchi na mifumo na iwapo uchafu na uovu huu utaenea katika serikali, basi kutakuwa na zilzala haribifu na yenye kutoa pigo kubwa kwa uhalali wa serikali hizo. Kwa hivyo, kuwepo uadilifu na kupambana na ufisadi ni nukta muhimu sana kwa mfumo kama wa Jamhuri ya Kiislamu ambao unahitaji uhalali ambao ni mkubwa zaidi kuliko uhalali wa kawaida unaohitajika na serikali nyingine."