Iran yamnyonga jasusi wa Mossad na CIA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i62307-iran_yamnyonga_jasusi_wa_mossad_na_cia
Hukumu ya kumnyonga jasusi wa Shirika Kuu la Kijasusi la Marekani CIA, na Shirika la Kijasusi la Utawala wa Kizayuni wa Israel, Mossad, imetekelezwa leo asubuhi,
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 20, 2020 02:23 UTC
  • Iran yamnyonga jasusi wa Mossad na CIA

Hukumu ya kumnyonga jasusi wa Shirika Kuu la Kijasusi la Marekani CIA, na Shirika la Kijasusi la Utawala wa Kizayuni wa Israel, Mossad, imetekelezwa leo asubuhi,

Kwa mujibu wa taarifa, Mahmoud Mousavi Majd ambaye amepatikana na hatia ya kushirikiana na mashirika ya kijasusi ya CIA na Mossad, amenyongwa leo asubuhi nchini Iran.

Jasusi huyo alikuwa anapokea dola za Kimarekani mkabala wa kuyakabidhi mashirika hayo taarifa mbali mbali za kiusalama hasa zinazohusu Majeshi ya Iran, Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na mahala alipokuwa akiishi Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani. Kesi ya jasusi huyo ilikuwa inasikilizwa na Mahakama ya Mapinduzi ambayo iliamuru anyongwe.

Mousavi Majd alikamatwa Oktoba 10 mwaka 2018 na kesi yake ikaanza kusikilizwa katika Tawi la 15 la Mahakama ya Mapinduzi ya Kiislamu na hatimaye baada ya mahakama kumpata na hatia, hukumu yake ya kunyongwa ilitolewa Agosti 25 mwaka 2019.

Hukumu hiyo ya kunyongwa imepitia michakato kadhaa ya kisheria katika Mahakama ya Kilele ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo imeidhinisha utekelezwaji wake.