Sera imara za Iran; kuunga mkono amani na uthabiti wa Afghanistan
Iran inaunga mkono amani na uthabiti wa Afghanistan.
Muhammad Ibrahim Taherian Fard, mjumbe maalumu wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran katikka masula ya Afghanistan, Jumapili ya jana tarehe 27 Julai akitoa radimali kwa matamshi ya mjumbe maalumu wa Marekani katika masuala ya Afghanistan alisisitiza kuwa, Tehran inaunga mkono kupatikana amani na uthabiti nchini Afghanistan na inasisitiza juu ya kuwekwa jiwe la msingi la amani kwa mujibu wa matokeo ya mazungumzo baina ya Waafghani kwa uongozi wa Waafghani wenyewe.
Zalmay Khalilzad, mjumbe maalumu wa Marekani katika masuala ya Afghanistan hivi karibuni alidai kuwa, Iran haitoi himaya na uungaji mkono wa kutosha kwa ajili ya kupatikana amani na uthabiti nchini Afghanistan.
Kadhalika Taherian Fard amewanasihi na kuwataka viongozi wa Marekani kuwa na ufahamu na welewa kamili kabla ya kuzungumzia mitazamo ya viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na masuala ya kieneo na ya Afghanistan.
Kutokana na sababu zinazoeleweka Iran inaunga mkono tukio na hatua yoyote inayosaidia kupatikana amani na uthabiti wa kudumu nchini Afghanistan. Ni kwa muktadha huo ndio maana Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ilitoa taarifa katika radiamali yake kuhusiana na kutiwa saini makubaliano kati ya Marekani na kundi la wanamgambo wa Taliban na kutangaza kuwa: Makubaliano ya amani ya kudumu nchini Afghanistan yatafikiwa tu kupitia mazungumzo baina ya Waafghani wenyewe kwa ushiriki wa makundi ya kisiasa ya nchi hiyo likiwemo la Talibani na kwa kuzizingatia nchi jirani na nchi hiyo.
Mtazamo huu unatilia mkazo nukta mbili muhimu ambazo katika tathmini ya madia ya Zalmay Khalilzad, mjumbe maalumu wa Marekani katika masuala ya Afghanistan kuhusu kutounga mkono Iran mwenendo wa kupatikana amani ya kudumu nchini Afghanistan zina umuhimu mkubwa.
Nukta ya Kwanza: Sisitizo la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran juu ya udharura wa kufikiwa makubaliano baina ya makundi ya nchi hiyo kupitia mazungumzo ya wenyewe kwa wenyewe. Kwa hakika jambo hilo, ni utangulizi wa kupatikana amani ya kudumu nchini Afghanistan.
Nukta ya Pili: Kuzingatia masuala ya kisiasa na kiusalama ya nchi jirani na Afghanistan. Hii ni katika hali ambayo, lengo la Marekani ni kuleta anga ya kutoaminiana sambamba na kuzusha mifarakano katika uhusiano wa Afghanistan na mataifa jirani.
Thomas Johnson mwandishi wa kitabu cha Taliban Narratives ameashiria nafasi muhimu ya ushirikiano wa kieneo kwa ajili ya kupatikana amani na usalama nchini Afghanistan na kusema kuwa: Marekani haidiriki kwamba, pasi na kushirikishwa nchi za eneo ikiwemo Iran, haiwezekani kupatikana ufumbuzi wa muda mrefu kuhusiana na usalama wa Afghanistan. Kuna haja ya kufanya hima ili Afghanistan ibadilike na kuwa mshirika mwaminifu kwa ajili ya eneo na ulimwengu.
Marekani ingali inafanya harakati iliyo kinyume na wengine na ikiendesha siasa zake za kujionyesha imepelekea kuibuka mivutano na mapigano. Hatua ya Marekani ya kuunga mkono ugaidi, mizozo na kuendesha siasa za chuki na hasama dhidi ya mataifa ya eneo imepelekea kushadidi ukosefu wa amani, uthabiti na kuongezeka umasikini, vita na misimamo ya kufurutu ada.
Ni jambo lililo wazi kwamba, Marekani inafuatilia ili kuhalalisha uingiliaji wake wa masuala ya ndani ya Afghanistan. Hii ni katika hali ambayo, njia pekee athirifu kwa ajili ya kupatikana amani ya kudumu nchini Afghanistan ni mazungumzo baina ya mirengo na makundi mbalimbali ya nchi hiyo kwa usimamizi wa Umoja wa Mataifa.
Kwa msingi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sanjari na kuheshimu mamlaka ya kujitawala Afghanistan na ardhi yote ya nchi hiyo, imetangaza utayari wake wa kutoa msaada na uungaji mkono wa aina yoyote ile ili kuhakikisha amani, uthabiti na usalama vinarejea katika nchi hiyo.