Kutosalimu amri jamii ya kimataifa mbele ya matakwa ya kibabe ya Marekani
Jamii ya kimataifa haitasalimu amri mbele ya matakwa ya kibabe ya utawala wa Marekani na inachofuatilia Washington ni kitu ambacho hakina hakitakuwa na faida yoyote.
Sayyid Abbas Mousavi, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema jana katika mkutano wake na waandishi wa habari kwamba, Tehran inapinga mashinikizo ya Marekani dhidi ya mataifa mengine ya dunia yenye lengo la kuongezwa muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran. Kwa mujibu wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran vinapaswa kuondolewa ifikapo tarehe 18 Oktoba mwaka huu.
Baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kuiondoa nchi yake katika makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) mwezi Mei 2018, alirejesha vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran katika awamu mbili ambapo vitisho vyake dhidi ya mataifa na asasi za kibenki vilikwamisha kutekelezwa makubaliano hayo ya JCPOA na washirika wa makubaliano hayo.
Kwa sasa serikali ya Marekani imeazimia kutoa pigo la mwisho kwa makubaliano ya JCPOA ili kwa hatua hiyo na kwa upande mmoja ibadilishe maafikiano hayo na kuyaonyesha kuwa, ni makubaliano yasiyo na faida kwa pande zilizobakia katika makubaliano hayo; na kwa upande wa pili ionyeshe kuwa, hatua yake hiyo ni mafanikio ya sera za kigeni za Washington na hivyo kuitumia hiyo kama kura ya turufu katika kampeni za uchaguzi ujao wa Rais Novemba mwaka huu.
Hata hivyo ili wafikie lengo hilo, viongozi wa Ikulu ya Marekani White House wanakabiliwa na changamoto kubwa na ndio maana wamekumbatia kila aina ya urongo na uzushi wakifanya juhudi za kuyaridhisha mataifa mengine ya dunia yakubaliane na mpango wao wa kutaka kuongezwa muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran. Viongozi wa Marekani wamekwenda mbali zaidi ambapo wamefikia hatua hata ya kuyatishia na kuyashinikiza mataifa mengine yaridhie mpango wake huo.
Brian Hook, mjumbe maalumu wa Marekani katika masuala ya Iran Jumapili iliyopita alizionya China na Russia akiziambia kwamba, kama zitaendelea na juhudi zao za kukwamisha kuongezwa muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa basi zitakabiliwa na hali ya kutengwa.
Tukiutazama utendaji huu wa kindumakuuwili wa Marekani ambao ni matokeo ya moja kwa moja ya sera za uchukuaji maamuzi kwa upande mmoja tunapaswa kuzingatia mambo matatu muhimu.
Jambo la Kwanza: Njama za kudhibiti nguvu za kiulinzi za Iran zinazofanyika kwa kutumia njia ya kudhoofisha uwezo wa makombora yake ni katika fremu za sera za Washington kueneza hofu, chuki na woga dhidi ya Iran (Iranophobia) katika eneo hili la Asia Magharibi.
Jambo la Pili: Kuibua changamoto katika uhusiano wa kawaida wa Iran kimataifa katika uga wa ushirikiano wa kijeshi kunafanyika kwa kutumia wenzo wa vikwazo vya silaha.
Jambo la tatu kwamba, kwa nini Marekani inazuia kuondolewa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran ni kuwa, Marekani inataka kuthibitisha ukubwa na ubwana wake wa maamuzi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hatua ambayo kama itatimia bila shaka itakuwa ni kulifanyia mzaha na kulicheza shere baraza hilo na misingi inayotawala katika mahusiano ya kimataifa.
Ni jambo lililo wazi kwamba, Iran kama ilivyo nchi nyingine yoyote ile ina haki ya kutetea haki zake za kisheria. Ni kwa kuzingatia uhakika huo ndio maana mkakati wa Iran umekuwa ni kuviimarisha vikosi vyake vya ulinzi kwa kutumia vifaa vya kiulinzi na wataalamu wazawa. Suala la kununua vifaa vya kijeshi kutoka mataifa mengine nayo ni haki ya Iran, na Marekani haina uwezo wa kulipokonya taifa hili haki hiyo kwa kutumia uongo na mashinikizo ya vikwazo.
Tajiriba inaonyesha kuwa, wenzo wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran hauwezi kuwa na faida kwa serikali ya Marekani.
Alaa kulli haal, katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, Iran imetoa tahadhari za lazima kwa mataifa na jamii ya kimataifa kwamba, endapo zitafuata sera za kibabe za Marekani na kutia dosari haki za kisiasa zilizoanishwa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA basi taifa hili litachukua hatua mkabala dhidi ya uamuzi huo.