Iran yakaribisha mkutano wa makundi ya Wapalestina huko Beirut
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i63239-iran_yakaribisha_mkutano_wa_makundi_ya_wapalestina_huko_beirut
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kikao cha pamoja cha makundi ya Wapalestina kilichofanyika katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut ni ishara kwamba viongozi wa Palestina wapo macho na wamesimama kidete mkabala wa utawala wa Kizayuni wa Israel pamoja na washirika wake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 05, 2020 06:45 UTC
  • Iran yakaribisha mkutano wa makundi ya Wapalestina huko Beirut

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kikao cha pamoja cha makundi ya Wapalestina kilichofanyika katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut ni ishara kwamba viongozi wa Palestina wapo macho na wamesimama kidete mkabala wa utawala wa Kizayuni wa Israel pamoja na washirika wake.

Saeed Khatibzadeh amesema hayo hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakaribisha kwa mikono miwili mkutano huo wa pamoja wa makundi ya Palestina.

Amesema mkutano huo wa Beirut umefikisha ujumbe wa wazi kwa walimwengu kwamba, Wapalestina wamesimama bega kwa bega kwa shabaha ya kukomboa maeneo yao yote yanayokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.

Khatibzadeh ameeleza bayana kuwa, licha ya kushuhudia miongo kadhaa ya uvamizi, hujuma, mzingiro na mauaji ya halaiki, wananchi wa Palestina wamethibitisha kuwa kamwe hawatoliweka pembeni suala la kuikomboa ardhi yao inayokaliwa kwa mabavu.

Mkutano wa Wapalestina Beirut

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, mataifa na serikali zingine duniani zilizokhitari muqawama na uhuru, zitaandamana na Wapalestina katika safari yao ya kuhakikisha kuwa wanafikia malengo yao.

Makatibu Wakuu na viongozi wa harakati 14 za Palestina wameshiriki kwenye kikao hicho cha Beirut huku Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina akihutubia kikao hicho cha kistratajia kutokea mji wa Ramallah katika Ukanda wa Gaza kwa njia ya video.