Sep 11, 2020 08:12 UTC
  • Zarif amhutubu Trump: Hakuna vita vibaya na vita vizuri

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemhutubu Rais Donald Trump wa Marekani na kumwambia kwamba, hakuna kitu kinachofahamika kama vita vizuri, na kusisitiza kuwa vita vyote ni vibaya.

Mohammad Javad Zarif amesema hayo katika ujumbe wake alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kufafanua kuwa, "Tunafahamu! Trump anadhania vita baridi ni vizuri kwa biashara, lakini vita moto si vizuri. Vita vyote ni viabaya! Basi!"

Dakta Zarif amekosoa misimamo ya kukinzana ya Trump ambapo kwa upande mmoja anasema vita ni vibaya, na kwa upande mwingine anaziuzia silaha kwa wingi nchi fulani za Asia Magharibi.

Ameeleza bayana kuwa, katika hali ambayo Donald Trump anakiri uchu wa Marekani wa kujaza mifuko ya kampuni za Marekani zinazouza silaha, binafsi amekuwa akishughulishwa zaidi na mwenendo wa kurundika eti 'silaha za kupendeza' za US katika eneo la Asia Magharibi.

Ujumbe wa Twitter wa Zarif akimhutubu Trump

Akizungumza katika Ikulu ya White House mapema jana, Trump alimkosoa mshindani wake katika uchaguzi mkuu wa urais wa mwaka huu, Joe Biden eti kwa kutuma vijana (wanajeshi) wa Marekani kupigana vita vya kiwendawazimu na visivyokwisha Asia Magharibi, akiwa Makamu wa Rais Barack Obama.

Aidha Trump aliikosoa vikali Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) kwa kuchochea vita kwa lengo la kuzinufaisha kampuni za nchi hiyo ya kibeberu zinazozalisha na kuuza silaha za kijeshi.

Tags