Iran: Makubaliano yoyote hayatodumu mpaka yatekeleze sawa haki na majukumu
(last modified Thu, 17 Sep 2020 02:22:46 GMT )
Sep 17, 2020 02:22 UTC
  • Iran: Makubaliano yoyote hayatodumu mpaka yatekeleze sawa haki na majukumu

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya haki za kimataifa amesema kuwa, makubaliano yoyote yale ya kimataifa hayawezi kudumu bila ya kuweko mlingano sawa katika utekelezaji wa haki na majukumu, na kwamba mapatano ya nyuklia ya JCPOA nayo hayawezi kutoka kwenye msingi huo.

Mohsen Baharvand alisema hayo jana Jumatano katika kikao cha Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA, mjini Vienna Austria na kubainisha msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu mapatano hayo ya nyuklia akisema: Isitarajiwe kwamba Iran itekeleze majukumu yake yote ndani ya JCPOA bila ya kupata haki zake zilizoainishwa kwenye maafikiano hayo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aidha ameuliza swali akisema: Je, JCPOA na ukaguzi unaofanywa na IAEA nchini Iran kwa mujibu wa mapatano ya JCPOA ni mambo ambayo yataendelea hivi hivi? Amejibu swali hilo akisema: Jawabu ni ndiyo lakini kwa sharti kwamba wajumbe wa jamii ya kimataifa wasimame imara kukabiliana na siasa za kibeberu za Marekani na wachunge thamani, mambo muhimu na haki za mataifa yote.

Mapatano ya nyuklia ya JCPOA

 

Vile vile amegusia udharura wa kuweko mlingano sawa baina ya haki na ahadi za Iran na kukumbusha kuwa, kwa mujibu wa mapatano hayo, Umoja wa Ulaya pamoja na nchi tatu za Ujerumani, Uingereza na Ufaransa na wajumbe wengine wa JCPOA kila mmoja ana wajibu wa kutekeleza vilivyo na inavyotakiwa ahadi zake katika makubaliano hayo.

Aidha amesema, hakuna mapatano mengine yoyote ya nyuklia yanayoweza kushika nafasi ya JCPOA na kusisitiza kuwa, Marekani imepoteza moyo na uwezo wa kuonesha njia za utatuzi wa matatizo ya kimataifa.

Tags