Iran na Uturuki zasisitiza kuimarisha ujirani mwema na wa kiudugu
(last modified Sun, 13 Dec 2020 07:38:55 GMT )
Dec 13, 2020 07:38 UTC
  • Iran na Uturuki zasisitiza kuimarisha ujirani mwema na wa kiudugu

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Uturuki wametilia mkazo umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kiudugu na ujirani mwema baina yao.

Mevlüt Çavuşoğlu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki usiku wa kuamkia leo amempigia simu waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Dk Mohammad Javad Zarif na kumuhakikishia kwamba Ankara inalipa umuhimu mkubwa suala la kuwa na uhusiano mzuri, wa kiurafiki na wa kiudugu na Tehran.

Vile vile amesema, Rais wa Uturuki anaheshimu haki ya kujitawala taifa na ardhi yote ya Iran na wala hakuwa na taarifa kuhusu hisia kali ambazo zingeliweza kujitokeza kupitia beti za shairi zilizosomwa. Anasema, beti hizo zilihusiana na eneo la Nagorno-Karabakh na Lachin na ndio maana zimesomwa katika sherehe zilizofanyika mjini Baku.

Kwa upande wake, Dk Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amehimiza kudumishwa uhusiano wa kiudugu na kuheshimiwa haki ya kujitawala ya nchi hizi mbili akisisitiza kuwa, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ana uhusiano mzuri na wa kiurafiki sana na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mapigano ya eneo la Nagorno-Karabagh

 

Ameelezea matumaini yake kwamba uhusiano wa Tehran na Ankara utazidi kuwa imara kwa kuimarisha anga ya kuaminiana na kuheshimiana baina ya pande mbili.

Siku ya Alkhamisi ya tarehe 10 Disemba, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki alisoma beti za shairi katika sherehe za ushindi wa eneo la Nagorno-Karabakh mjini Baku Azerbaijan zilizohusiana na Mto Aras ambazo zilionekana zinachochea fikra za kujitenga baadhi ya maeneo ya Iran.

Balozi wa Uturuki mjini Tehran Ijumaa aliitwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran na kutakiwa Ankara itoe majibu ya haraka na ya wazi kuhusu beti hizo alizosoma Erdogan katika sherehe hizo.