Khatibzadeh: Hakutakuweko mazungumzo ya pande mbili baina ya Iran na Marekani
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, taifa hili halitafanya mazungumzo na serikali ya Marekani.
Saeed Khatibzadeh amesema hayo leo katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari ambapo sambamba na kuashiria kwamba, Iran inasubiri Marekani ichukue hatua kuhusiana na kuliondolea taifa hili vikwazo vyote ameeleza kuwa, serikali ya Washington inapaa kutekeleza ahadi zake na kama itafanya hivyo, basi kutakuwa na uwezekano wa kufanyika mazungumzo katika fremu ya Kamisheni ya Pamoja ya makubaliano ya nyujlia ya JCPOA.
Khatibzadeh ameongeza kuwa, subira ya kistarejia ya Iran pamoja na hatua zake ilizochukua kwa mujibu wa vipengee nambari 26 za 36 vya JCPOA zimepelekea kubakia hai makubaliano hayo ya kimataifa.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia sera na siasa za Iran katika eneo la Caucasia na kubainisha kwamba, siasa za kieneo za Tehran ni za ujirani mwema na eneo hilo tangu kale limekuwa na umuhimu kwa Jamhuri ya Kiislamu.
Ameashiria safari ya ujumbe wa kundi la Taliban hapa nchini na kusema, kuwa, serikali ya Afghanistan ilikuwa na taarifa kamili kuhusiana na safari hii. Kadhalika amesema, Iran inaunga mkono mazungumzo baina ya Waafghani ambapo Taliban ni sehemu ya jamii ya nchi hiyo.
Khatibzadeh amezungumzia pia vitisho vya utawala haramu wa Israel dhidi ya Iran na kusema kuwa, taifa hili halina ada na mazoea ya kutoa vitisho, lakini wakati wowote itakapolazimu, basi litatoa jibu mwafaka na la mahala pake.