Feb 02, 2021 03:46 UTC
  • Zarif: Marekani sharti itekeleze wajibu wake kwa kurejea katika JCPOA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Marekani haina budi kutekeleza wajibu na majukumu yake kwa kurejea katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Katika mahojiano maalumu na kanali ya televisheni ya CNN ya Marekani jana jioni, Muhammad Javaz Zarif amesema Washington inapaswa kujiandalia mazingira ya kurejea katika JCPOA kwa kuwa yenyewe ilichukua uamuzi wa kujiondoa kwenye mapatano hayo ya kimataifa.

Dakta Zarif ameeleza bayana kuwa, "Iran imetumia kipengee cha makubaliano hayo kupunguza uwajibikaji wake. Ukisoma kipengee cha 36 cha JCPOA, Tehran imekitumia kwa mujibu wa mapatano hayo." Ameongeza kuwa, Iran ililazimika kupunguza uwajibikaji wake katika JCPOA baada ya Marekani kuanzisha vita kamili vya kiuchumi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Ameeleza bayana kuwa, kama ambavyo washiriki wa mapatano hayo hawakukubali masharti fulani kabla ya kusainiwa mapatano hayo, kwa mfano Marekani ilikataa suala la mauzo ya silaha zake kwa nchi za eneo lijadiliwe, vivyo hivyo Iran haitakubali masharti mapya ya Washington ya kurejea kwenye mapatano hayo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, uwezo wa kiulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu si sehemu ya makubaliano hayo na kwamba iwapo Washington inataka hayo yajadiliwe, basi itangaze pia kuwa iko tayari kusimamisha mauaji ya watoto wadogo na wanawake nchini Yemen, na vile vile itaacha kurundika silaha zake katika nchi za eneo la Asia Magharibi.

Dakta Zarif katika mahojiano na CNN kupitia mtandao wa Skype

Kuhusu mvutano uliopo baina ya Washington na Tehran juu ya kurejea katika mapatano hayo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amebainisha kuwa, Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya kama mshirikishi mkuu wa JCPOA anapaswa kutumia wadhifa huo kuupatia ufumbuzi mvutano huo.

Ameongeza kuwa, 'wakati' si suala muhimu kwa sasa, na kwamba jambo la dharura la kupigwa darubini kwa sasa ni kuona iwapo utawala mpya wa Marekani wa Joe Biden utaendelea kufuata sera zilizofeli za Donald Trump au la.

Tags