Rouhani: Iran haijaona nia njema ya utawala mpya wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i66740-rouhani_iran_haijaona_nia_njema_ya_utawala_mpya_wa_marekani
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema taifa hili halijashuhudia nia njema wala mabadiliko ya kivitendo ya sera za Marekani mkabala wa Jamhuri ya Kiislamu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 11, 2021 12:29 UTC
  • Rouhani: Iran haijaona nia njema ya utawala mpya wa Marekani

Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema taifa hili halijashuhudia nia njema wala mabadiliko ya kivitendo ya sera za Marekani mkabala wa Jamhuri ya Kiislamu.

Rais Rouhani amesema iwapo utawala mpya wa Washington una azma ya kweli ya kutimiza ahadi zake, basi unapaswa kufuata mkondo mpya na urekebishe makosa yaliyofanywa na utawala uliopita dhidi ya Iran.

Dakta Rouhani amesema serikali mpya ya Marekani imeacha kubwabwaja na kutoa matamshi ya uhasama dhidi ya taifa hili lakini haijachukua hatua zozote za maana kivitendo.

Rais wa Iran ameeleza bayana kuwa, "ni bora utawala mpya wa Marekani usifuate njia ya gaidi mkubwa (Trump) ambaye alikuwa fedheha kwa nchi yake na kwa dunia nzima."

Rais Joseph Biden wa Marekani

Amebainisha kuwa, serikali ya Joe Biden inapaswa kutambua kuwa, dunia nzima hivi sasa inafahamu bila chembe ya shaka kuwa vita vya kiuchumi na sera za mashinikizo ya Marekani dhidi ya wananchi wa Iran zimegonga mwamba.

Kuhusu kampeni ya kuwapiga chanjo ya Covid-19 wananchi wa Iran, Dakta Rouhani amesema anatumai kuwa, watu wote walioko katika hatari ya kukumbwa na maradhi hayo wakiwemo wahudumu wa afya na wazee watapata chanjo hiyo kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa Kiirani, na mpango wa kuwachanja wananchi wengine wote kwa makundi utaanzia mapema mwaka ujao wa 1400 Hijria Shamsia (kuanzia Machi 21).