Zarif: Marekani inapaswa kuondoa bila masharti yoyote vikwazo vyote vilivyowekwa na Trump
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, Marekani inapaswa kuondoa bila masharti yoyote na kwa namna iliyo athirifu vikwazo vyote vilivyorejeshwa upya na kutekelezwa na aliyekuwa rais wa nchi hiyo Donald Trump.
Mohammad Javad Zarif ametoa sisitizo hilo leo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa twitter, likiwa ni jibu kwa hatua ya Marekani ya kulegeza msimamo kwa kufuta uamuzi wake wa kutekeleza kanuni ya kurejesha kwa mpigo vikwazo vyote vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran.
Amesema: "Marekani imekiri kuwa madai ya Pompeo kuhusu azimio 2231 hayana itibari yoyote kisheria; na sisi tunaafiki."
Dakta Zarif ameongeza kuwa, katika kuheshimu na kutekeleza azimio 2231, Marekani inapaswa kuondoa bila masharti yoyote na kwa namna iliyo athirifu vikwazo vyote vilivyorejeshwa upya na kutekelezwa na aliyekuwa rais wa nchi hiyo Donald Trump.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, baada ya kuondolewa vikwazo na Marekani, Iran nayo itarejesha haraka katika hali yake ya awali hatua zote rekebishi (za kupunguza uwajibikaji katika JCPOA) ilizokuwa imechukua.
Mnamo Agosti 2020 na baada ya kushindwa kurefusha vikwazo vya silaha dhidi ya Iran, serikali ya aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump ilianzisha harakati zilizogonga mwamba pia za kutaka kurejesha tena vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran.
Hivi sasa serikali mpya ya Marekani, ambayo imebainikiwa na kufeli kwa sera za serikali iliyotangulia ya nchi hiyo katika kutekeleza vikwazo vya juu kabisa dhidi ya Iran, imetangaza kwamba kwa kutilia maanani kuwa hatua ya upande mmoja ya kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA imepelekea kutengwa kimataifa, Washington inaamua kurudi kwenye makubaliano hayo yaliyoidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na kuondoa vikwazo vya umoja huo dhidi ya Iran.../