Iran: Wamarekani wawajibike kuhusu jinai wanazofanya huko Yemen, waache bwabwaje
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran amesema kuwa Wamarekani wanapaswa kuwajibika kutokana na jinai na uhalifu wao wa miaka 6 sasa huko Yemen badala ya kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya nchi nyingine.
Saeed Khatibzadeh ambaye alikuwa akizungumzia tuhuma zisizo na msingi zilizotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kuhusu hali ya Yemen amesema kuwa: Wavamizi na maadui wa taifa la Yemen ambao wamekuwa wakiwaua kwa umati wananchi wasio na hatia kwa kipindi cha miaka sita iliyopita, kupora maliasili na kuharibu miundombinu ya nchi hiyo, wanaelewa vyema kwamba wamefeli na kushindwa mbele ya taifa ngangari la Yemen katika stratijia yao ya kijeshi iliyo dhidi ya binadamu, na sasa wanataka kujivua hatia ya kuhusiana na jinai hizo kwa kutoa tuhuma zisizo na msingi na kuzipotosha fikra za walimwengu.
Khatibzadeh amesema, serikali mpya ya Marekani imeendeleza misimamo isiyo sahihi ya serikali ya kabla yake kwa kutoa tuhuma zisizo na msingi na kufumbia macho ukweli wa mambo huko Yemen na kuongeza kuwa: Madai ya Marekani kwamba inataka kurejesha amani nchini Yemen ni maneno matupu, na Washington imetosheka na mchezo wa kisiasa katika kadhia hii.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran amesema tangu mwanzoni mwa vita vya Yemen Iran ilikuwa isisitiza kuwa, mgogoro huo hauwezi kutatuliwa kwa njia za kijeshi. Ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetumia uwezo wake wote kwa ajili ya kusaidia jitihada za Umoja wa Mataifa za kurejesha amani nchini Yemen na inaunga mkono jitihada zote za kukomesha kabisa mashambulizi dhidi ya taifa hilo.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Antony Blinken amedai kuwa harakati ya Ansarullah ya Yemen inaendelea kutumia silaha, taarifa, mafunzo na misaada ya Iran kufanya mashambulizi yanayotishia maeneo ya kiraia na mindomsingi ya Yemen na Saudi Arabia.