'Hayatafanyika mazungumzo yoyote bila Marekani kuondoa vikwazo vyote dhidi ya Iran'
(last modified Mon, 08 Mar 2021 08:05:38 GMT )
Mar 08, 2021 08:05 UTC
  • 'Hayatafanyika mazungumzo yoyote bila Marekani kuondoa vikwazo vyote dhidi ya Iran'

Duru moja ya kuaminika ya kiusalama nchini imetangaza kuwa: hakuna mazungumzo yoyote na katika sura yoyote yatakayofanyika baina ya Iran na Marekani bila kuondolewa kwanza vikwazo vya Washington dhidi ya Tehran.

Kwa mujibu wa duru hiyo ya kiusalama ya Iran, Wamagharibi wameyatafsiri kimakosa matamshi ya hivi karibuni ya Rais Hassan Rouhani kwamba Marekani irudi kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA baada ya kuchukua hatua za kivitendo na ikabainisha kuwa, hakuna mpango wowote mpya kwa ajili ya kufanyika mazungumzo kati ya Iran na Marekani.

Duru hiyo imeongeza kuwa, wazo la mpango wa utekelezaji mambo hatua kwa hatua kwa ajili ya kuanza mazungumzo baina ya Marekani na Iran limekataliwa katika ngazi za juu kabisa za Jamhuri ya Kiislamu; na bila kutangulia kuondolewa vikwazo, hakuna mawasiliano yoyote yatakayofanywa kati ya Iran na Marekani.

Siku ya Alkhamisi iliyopita na katika hotuba aliyotoa kwa njia ya intaneti kwenye kikao cha 14 cha wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ECO kilichohudhuriwa na viongozi wa nchi 10 wanachama, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema, Marekani ina wajibu wa kurudi kwenye makubaliano ya JCPOA kwa kuondoa vikwazo vyote na kuchukua hatua za kivitendo, kwa sababu hilo ni jukumu la nchi iliyokiuka ahadi na majukumu yake.../

 

Tags