Qalibaf: Ni lazima Marekani iondoe vikwazo vyote dhidi ya Iran
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema: "Marekani inapaswa kuondoa vikwazo vyote ili Iran iweze kutekeleza ahadi zake katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA."
Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Bunge la Iran ameyasema hayo katika mahojiano na Kanali ya Pili ya Televisheni ya Iran na kuongeza kuwa mapatano ya JCPOA ni ya kimataifa na yameidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Ameongeza kuwa, tuliona namna ambavyo baada ya kuidhinishwa JCPOA si tu kuwa Marekani haikutekeleza ahadi zake katika mapatano hayo, bali pia, kinyume na sheria za kimataifa, ilitoa vitisho dhidi ya watu wa Iran katika zama za utawala wa Trump.
Qalibaf amesema sheria iliyopasishwa na bunge ya 'hatua za kistratijia kwa ajili ya kuondolewa vikwazo na kulinda haki za taifa la Iran; imepelekea Wamarekani wafahamu kuwa, si Iran tu inayopaswa kutekeleza ahadi zake bali wao nao pia wanapaswa kutekeleza waliyoyaahidi katika JCPOA.
Amesema sheria hiyo ya bunge la Iran ni dhihirisho la nguvu na uwezo wa Iran na inatoa fursa ya kufanyika mazungumzo na kuondolewa vikwazo.
Aidha amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi kukiuka mapatano ya JCPOA bali ni upande wa pili ndio umekuwa ukikuka mapatano hayo ya kimataifa.