Araqchi: Mkutano wa Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA Vienna ni chanya
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa ameashiria kuhusu mkutano wa jana Jumanne mjini Vienna wa Kamisheni ya Pamoja ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kusisitiza kuwa, muelekeo wa kikao hicho ni chanya na wenye kutia matumaini.
Sayyid Abbas Araqchi amesema hayo katika mahojiano na kanali ya Press TV baada ya mkutano huo na kuongeza kuwa, mazungumzo hayo ya washiriki wa Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA yataendelea Ijumaa ijayo.
Mwakilishi huyo wa Iran katika mkutano huo wa Vienna amesisitiza kuwa, mazungumzo hayo yamejikita juu ya kurudi Iran katika utekelezaji kamilifu wa JCPOA, mkabala wa kuondolewa vikwazo vyote kwa mkupuo.
Ameeleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu haitakubali kuondolewa vikwazo haramu na vya kidhalimu hatua kwa hatua mkabala wa kurejea katika utekelezaji kamili wa majukumu yake iliyoyapunguza kama jibu la vikwazo haramu na hatua ya upande mmoja ya Marekani ya kujiondoa kwenye mapatano hayo ya kimataifa.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amesema iwapo Marekani inataka kweli kurejea katika makubaliano hayo, basi haina budi kuliodolea taifa hili vikwazo vyote kwa mkupuo.
Kadhalika Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amesisitiza kuwa, mazungumzo hayo ya Vienna ya Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA yanaihusu tu Iran na kundi la 4+1, na kwamba hakutakuwa na mazungumzo yoyote ya ana kwa ana au yasiyo ya ana kwa ana na Marekani juu ya JCPOA, au hata masuala mengine.