Iran haitaruhusu mazungumzo ya Vienna kuhusu JCPOA yawe marefu kupita kiasi
(last modified Wed, 21 Apr 2021 07:32:40 GMT )
Apr 21, 2021 07:32 UTC
  • Iran haitaruhusu mazungumzo ya Vienna kuhusu JCPOA yawe marefu kupita kiasi

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amesema Jamhuri ya Kiislamu haitamruhusu yeyote ayageuze mazungumzo ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yanayofanyika huko Vienna, mji mkuu wa Austria kuwa marefu kupita kiasi na yasiyo na kikomo.

Sayyid Abbas Araqchi alisema hayo jana Jumanne baada ya kumalizika duru nyingine ya mkutano wa Kamati ya Pamoja ya JCPOA na kusisitiza kuwa, kila nukta ya mazungumzo hayo inafuatiliwa kwa jicho la karibu sana na Iran.

Amesema kikao cha jana kilikuwa kilele cha mazungumzo ya siku sita zilizopita, na kilijikita zaidi kuhusu hatua za kivitendo zinazopaswa kuchukuliwa na Marekani kwa ajili ya kuliondolea taifa hili vikwazo vya kidhalimu.

Sayyid Araqchi ameeleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itarejea tena katika utekelezaji kamilifu wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA baada ya Marekani kuondoa vikwazo vyote kivitendo, na si kwa maneno matupu au kwa maandishi tu.

Mazungumzo ya Vienna

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amebainisha kuwa, Iran kamwe haitapuuza masuala muhimu kwa kuharakishwa mazungumzo hayo, na wakati huo huo haitaruhusu mazungumzo hayo yawe marefu kupita kiasi.

Huku hayo yakiarifiwa, duru zilizo karibu na mazungumzo hayo zimeiambia kanali ya Press TV kuwa, Iran katu haitaruhusu kusimamishwa, kulegezwa au kuondolewa vikwazo hatua kwa hatua.

Iran inasisitiza kuwa vikwazo hivyo vinapaswa kuondolewa vyote kwa mkupuo, na kisha ipewe miezi mitatu hadi sita kuthibitisha kuwa vikwazo hivyo vimefutwa kweli.

Tags