Apr 27, 2021 13:13 UTC
  • Rais Rouhani asisitiza haja ya kuimarishwa uhusiano wa Iran na Afrika Kusini

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametilia mkazo suala la kuimarishwa uhusiano wa pande mbili wa taifa hili na Afrika Kusini katika nyuga anuai.

Rais Rouhani ametoa mwito huo katika ujumbe wake aliomtumia mwenzake wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Taifa ya nchi hiyo ya Kiafrika.

Sanjari na kutoa mkono wa pongezi kwa Rais Ramaphosa, serikali yake na taifa la Afrika Kusini kwa ujumla kwa mnasaba wa siku hii muhimu katika historia ya nchi hiyo, Dakta Rouhani amesema anatumai kuwa nchi hiyo itaondokana na janga la virusi vya Corona liliyoisakama.

Rais wa Iran amebainisha kuwa: Dunia hii leo inakabiliwa na migogoro mingi ikiwemo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, na mripuko wa janga la Corona umefanya matatizo hayo kuongezeka maradufu. Natumai nchi mbili hizi zitashirikiana katika kupambana na janga hili.

Hayati Nelson Mandela, shujaa wa mapambano dhidi ya mfumo wa Apartheid

Dakta Hassan Rouhani amesisitizia udharura wa kunyanyua kiwango cha ushirikiano na uhusiano baina ya nchi mbili hizi rafiki katika nyuga mbalimbali kwa maslahi ya pande mbili.

Wananchi wa Afrika Kusini leo Aprili 27 wanaadhimisha siku waliojikomboa toka kwenye minyororo ya mfumo wa ubaguzi (apartheid), na uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia kufanyika nchini humo.

 

Tags